Wachina 3 wamekamatwa na polisi wiki iliyopita huko Kunasi katika mkoa wa Ashanti nchini Ghana kwa kugeuza nyumba 'apartment' walimokuwa wamepanga kuwa mgodi wa dhahabu ambazo walikuwa wakizichimba.
Kutokana na maelezo ya mwenye nyumba yanasema kuwa wachina hao walipanga nyumba hiyo mwaka jana na walikuwa wakichimba dhahabu kwa kipindi chote hicho bila yeye mwenyewe kufahamu mpaka mpangaji mwingine alipokuja kumwambia.
Wachina hao walipohojiwa na kuulizwa walijuaje kuwa ndani humo kulikuwa na dhahabu, walisema kuwa mwanzo walipokodi nyumba hiyo alikuwa lengo lao kuchimba dhahabu, ila walikuwa na ardhi ambayo waliingia mkataba kuchimba dhahabu.
Waliendelea kusema kuwa, walipoingia ndani humo, vifaa walivyokuwa wavitumie kuchimbia eneo lenye mkataba walivitunza ndani humo na kimoja kati ya hivyo ambacho ni cha kugundua dhahabu 'Gold Detector' kilianza kugundua kuwa ndani humo kulikuwa na dhahabu ya kutosha.
Akizungumza jirani aliyewagundua, yeye alisema kuwa alikuwa akiwaona wachina hao kila usiku wakitutusa viroba vya udongo na kuvitupia mbali kidogo na nyuma ya nyumba hiyo, ndipo alipoamua kumuita mwenye nyumba na kuwakamata.
Wakati mwenye nyumba alipokuja kugundua, walishachimba eneo kubwa mno na walishavuna dhahabu nyingi mno ambayo ilitumiwa kama ushahidi.