Sunday, 13 April 2014

Athari za mvua zaendelea kutesa raia Dar na mikoa ya jirani.

Mvua iliyoanza kunyesha mwishoni mwa wiki, imeendelea kuleta kizaazaa katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo kusababisha maelfu ya abiria kukwama kusafiri kati ya Dar es Salaam na mikoa mingine kupitia Barabara ya Morogoro.

Mawasiliano yalikatika kutokana na daraja la mto Ruvu, kuzingirwa na maji na lingine lililoko eneo la Visiga, kingo zake kutitia.

Licha ya athari katika miundombinu zilizosababisha magari na abiria kusota katika eneo hilo la Ruvu mkoani Pwani kwa zaidi ya saa 12, kwa upande wa Mkoa wa Morogoro vifo viwili vimeripotiwa kutokea baada ya watu wawili kufunikwa na maporomoko ya udongo, yaliyosababishwa na mvua.

Wakati Rais Jakaya Kikwete alikwenda kutembelea maelfu ya abiria waliokwama kwenye daraja la Ruvu, kwa upande wa Dar es Salaam hali iliendelea kuwa tete, kutokana na nyumba kadhaa kuzingirwa na maji.

Katika harakati za kutaka kwenda kukagua athari za mafuriko katika Jiji la Dar es Salaam, Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal na viongozi wengine, walinusurika kifo baada ya helikopta waliyotaka kuitumia kuanguka.

Viongozi wengine waliokuwamo kwenye helikopta hiyo ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki na Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.

Rais Jakaya Kikwete pamoja na mkewe, Mama Salma Kikwete na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza wakikagua mafuriko yaliyoharibu vibaya barabara ya Chalinze hadi Dar es Salaam, eneo la Ruvu Darajani jana. Mamia ya abiria walikwama kutokana na mafuriko hayo.