Tuesday, 11 March 2014

Waswekwa ndani saa 3 kwa kuvaa vimini.

Wanawake wawili Jumatatu walizuiliwa kwa saa 3 na mahakama moja nchini Uganda kwa kuingia mahakamani wakiwa wamevalia 'Mini Skirt'.

Hii ni baada ya jaji aliyekuwa mahakamani humo kusema kuwa wanawake hao walikuwa wamevalia
nguo zisizofaa.

Kwa mujibu wa taarifa kwenye mtandao wa Daily Nation, nchini Kenya, Bi Prosy Nasuna aliyekuwa
amemshitaki Bi Jane Nabukenya kwa kukosa kumlipa deni lake la shilingi milioni 3 za Uganda
wote walisemekana kutovalia nguo za heshimana kutatiza kikao cha mahakama.

Walipoingia mahakamani katika eneo laBukomansimbi wiki jana Prosy pamoja na mshitakiwa walijikuta matatani.

Kabla ya kuchukuliwa hatua kwa mavazi yao, watu walipiga mayowe mahakamani humo wakisema kuwa wawili hao walikuwa wamevalia visivyo kulingana na sheria iliyopitishwa mwezi jana kuhusiana na kupiga marufuku mavazi fupi.

Sheria hiyo inasema kuwa yeyote atakeyeonyesha sehemu za siri za mwili wake hadharani na
kusababisha hisia fulani miongoni mwa watu, anakuwa amekiuka sheria.

Minong'ono na kelele za watu zilisababisha hakimu kuamuru kukamatwa kwao kwa kwenda
kinyume na sheria na pia kwa kuhujumu mahakama.

Alisema kuwa kesi ilikosa kuendelea kutokana na
mavazi yao na kwa hivyo kosa lao lilikuwa kusababisha usumbufu mahakamani kwa kuvalia 'Mini Skirt'.

Hakimu aliwahukumu jela masaa 3 wanawake hao na kuahirisha kesi yao hadi tarehe 13 mwezi
Machi.