Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Addo November, jana aliwaongoza baadhi ya viongozi, wadau na waandishi wa habari kwenda kutoa mkono wa pole
nyumbani kwa msanii wa siku nyingi, Haji Noorah, ambaye alifanyiwa upasuaji wa tumbo Februari 20.
November akizungumza nyumbani kwa Noorah, alisema wadau wa muziki wanapaswa kujitokeza kumuona mgonjwa na kumchangia kwa hali na mali kadiri itakavyowezekana, kwani zinatakiwa sh milioni 2.7 kwa gharama za matibabu.
Alisema kuwe na utaratibu wa kuchangia wagonjwa si hadi wakati wa vifo, huku akimmwagia sifa mwanamuziki huyo kuwa siku zote amekuwa akiishi maisha ya kujiheshimu tofauti na ilivyo kwa
wasanii wengine ambao wamekuwa
wakiongozwa na kashfa.
Aliongeza kuwa Noorah alifanyiwa
upasuaji mara baada ya kuanguka ghafla na kugundulika kuwa utumbo wake ulikuwa umejisokota, jambo ambalo lilimfanya alazwe katika chumba cha wagonjwa mahututi na kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Kairuki,
Mikocheni jijini Dar es Salaam.
“Sisi kama Shirikisho la Muziki
tumefika hapa kumpa pole msanii
mwenzetu, pia tulitafuta wadau ili
tuweze kumpa chochote, hivyo
tunamkabidhi kiasi cha sh 500,000 tu, hivyo na wengine wakiweza wawasiliane na Shirikisho,” alisema November.
Aliwataja wadau waliochangia kuwa ni pamoja na Cosota ambao waliwakilishwa na Ofisa Usajili, Philemon Kilaka.
Akizungumza mara baada ya kupokea pole hiyo, Noorah alisema, analishukuru Shirikisho kwa moyo waliounesha kwake, huku akisisitiza kwa kuweka wazi jambo moja kubwa kwa jamii kuwa
na utaratibu wa ‘kucheki’ afya zao mara kwa mara na siyo kusubiri hadi waumwe.
“Jamii iweke utaratibu wa ‘Afya Check’ ili kuweza kujua magonjwa nyemelezi kabla, kama mimi nimekuwa na tatizo hili kwa miaka 20, nimekuwa nikiumwa sana tumbo lakini sikujua kama utumbo
ulikuwa unajisokota, nilijua ni vidonda vya tumbo kumbe wakati nilipokuwa napata maumivu makali utumbo ulikuwa
unajisokota, kama ningekuwa na
utaratibu wa kucheki afya yangu
ningegundua tatizo hili mapema,”
alisema Noorah.
Noorah aliwahi kutamba na ngoma zake kama, ‘The Baba Style’, ‘Vijimambo’, ‘Hantaki’, ‘Wameiba’, ‘Pombe’ aliomshirikisha Mez B, ‘Ice Cream’ aliomshirikisha Suma Lee, ‘Dem Kama Wewe’, ‘Ukanda wa Giza’, ‘Zai’ alioimba na Mwana FA, Mez B, Jay Moe, Feza Kessy na nyinginezo.