Usafiri wa pikipiki na bajaji kupigwa marufuku kufanya huduma zake katikati ya jiji la Dar es salaam kwa kile kinachodaiwa kuwa usafiri huo unachochea msongamano barabarani ambayo ni kero kwa mamlaka husika.
Meneja uhusiano wa mamlaka uthibiti wa vyombo vya usafiri nchi kavu na majini Tanzania, David Mzirai alisema wanatafuta dawa kuhakikisha hakuna kabisa bodaboda wala bajaji zinazozunguka katikati ya jiji.
"Tupo kwenye harakati za kuwatafutia dawa kuhakikisha hakuna anayeingia katikati ya jiji kabisa," alisema Mzirai.
Nae mwenyekiti wa shirikisho la pikipiki na bajaji Dar es salaam, Adam Yule alisema kuwa hata kama serikali inakataza usafiri huo usifike mjini bado tatizo la msongamano litakuwepo.
Aliongeza kuwa, nafasi ya usafiri wa bodaboda na bajaji katika kurahisisha usafiri bado itabaki pale pale kwa kuwa usafiri wa umma unaotegemewa haukidhi mahitaji.
"Usafiri wa Umma unaotegemewa kutatua tatizo la usafiri haukidhi mahitaji hata japo kwa 30%. Ukitembelea vituo kama vya Mbagara na Tegeta utaona raia wanavyohangaikia usafiri wa umma," alieleza Yule.