Watu wanne wanaosadikiwa kuwa
majambazi wakiwa na silaha wamevamia nyumba ya kulala wageni kijijini Mtowisa Bonde la Ziwa Rukwa, wilayani Sumbawanga
na kuwapora wafanya biashara ya ng'ombe zaidi ya Sh milioni 13 fedha taslimu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda amesema tukio hilo lilifanyika Machi 9 saa nne usiku kijijini Mtowisa katika nyumba ya kulala wageni iitwayo
Kaozye.
Mwaruanda alisema pamoja na kuanzisha msako wamewatia mbaroni watu watatu kwa
mahojiano kuhusu tukio hilo.
Majambazi hao walipofika katika nyumba hiyo awali walimuulizia mhudumu wa nyumba hiyo ya wageni aitwae Andrea Cherehani ambaye alifanikiwa kutoroka na
kujificha chumba cha nje katika nyumba hiyo ya kulala wageni.
"Walipofika (watuhumiwa) walitukuta tumekaa nje na wakadai kuwa tupo chini ya
ulinzi, walianza kuniulizia mimi (mhudumu), lakini waliponikosa wakapaza sauti na kusema kuwa wanahitaji wafanyabiashara hao wa ng'ombe na kusema hawataki
kuwaua ila walihitaji fedha walizokuwa nazo," alisema Cherehani.
Hata hivyo, baada ya wafanyabiashara haovkusikia hivyo hawakujitosa ndipo majambazi hao walipofyatua risasi kwenye paa la nyumba hiyo kabla ya kuingia kwenye vyumba vya nyumba hiyo ambapo waliwapata wafanyabishara wakawapiga,
kuwapora fedha zao na kutoweka
kusikojulikana.
Majambazi hao inadaiwa walipitia majina ya wageni waliofika siku hiyo kwenye nyumba hiyo ya wageni kama walivyojiorodhesha
kwenye kitabu cha wageni akiwemo Shija Rabandiye ambaye anadaiwa kuporwa fedha taslimu zaidi ya milioni 10, Masai Bumado
na Bakaga Edward ambao kwa pamoja waliporwa zaidi ya milioni tatu.
Mwaruanda alithibitisha kuwa
wafanyabiashara hao walikuwa wametokea eneo la Iyunga jijini Mbeya na kufika kijijini Mtowisa kwa ajili ya kununua ng'ombe
mnadani kwamba pamoja na fedha taslimu pia waliporwa simu nne za mkononi za aiana mbalimbali.
Mganga wa zamu wa Kituo cha Afya cha Mtowisa katika Bonde la Ziwa Rukwa, wilayani Sumbawanga, Linus Romani alikiri kuwapokea majeruhi wa tukio hilo ambapo
amedai kuwa walilazwa hapo usiku huo kwa matibabu na kuruhusiwa siku iliyofuata.