Thursday, 16 January 2014

TUWACHUNGE WATOTO WETU DHIDI YA MICHEZO HATARISHI.

Ukizungumzia michezo ya watoto unakuwa unazungumzia kitu ambacho ni muhimu sana kwa mtoto na ni haki pia ambayo kila mtoto anastahili kupewa na ikitokea mtoto ananyimwa haki hiyo basi unakuwa unamdhurumu haki yake ya msingi sana.

Waswahili wana msemo wao usemao, michezo ni afya ikimaanisha kwamba kama unajihusisha na michezo basi kwa namna moja hama nyingine utakuwa unaboresha afya yako, hivyo hivyo kwa watoto, wanatakiwa wapewe nafasi ya kucheza ili waweze kuimarisha afya zao.

Lakini pia michezo ya watoto inawasaidia kuzichangamsha akili zao na kuwafanya watoto wawe na uwezo mpana wa kifikiri vizuri ukilinganisha na wale ambao hawapewi haki hii ya msingi.

Katika kuwapa haki hii ya msingi,watoto hawa wanapaswa kuangaliwa kwa umakini juu ya michezo ambayo inaonekana dhahili kwamba inaweza kuhatarisha afya zao kiujumla. Suala hili la uangalizi linapaswa kuanzia kwa mzazi au mlezi wa mtoto husika na jamii kwa ujumla.

Michezo hatarishi kama ya kucheza juu ya miti ni michezo inayoweka afya za watoto matatani kufuatia ajali ambazo zinaweza kuwatokea kama vile kudondoka na kuvunjika baadhi ya viungo vya mwili na kusababisha ulemavu wa kudumu.

Jukumu la kuwalinda watoto wetu ni letu sote kwani waswahili wanasema, mtoto wa mwenzio ni wako,hivyo si vibaya tukichukua nafasi za wazazi au walezi katika kufanikisha jukumu la kulilinda taifa letu la kesho.