Sunday, 26 January 2014

NILIJUA NAENDA KUWA MWANAFUNZI, KUMBE MAMA NITILE.

Baada ya kumaliza elimu ya shule ya msingi miaka miwili iliyopita mkoani Iringa, akiwa na umri wa miaka 15 na kufanikiwa kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari, msichana huyo ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Onesta alichukuliwa na mama yake mdogo anayeishi Dar es salaam kwa ahadi ya kumtafutia shule bora.

Kwa matumaini makubwa msichana Onesta alikubali kuondoka na mama yake mdogo kuelekea Dar es salaam kwa lengo la kutafutiwa shule aliyoahidiwa.

Akizungumza kwa hisia, Onesta alisema kwamba alianza kuona ndoto zake za kwenda shule zinapotea taratibu baada ya kufika mjini na kuona akishirikishwa zaidi kwenye biashara aliyokuwa anaifanya mama yake mdogo na sio kama alivyokuwa anategemea.

Onesta alisema kwamba, pindi alipokuwa akimuulizia mama yake mdogo kuhusu suala la kumpeleka shule alikuwa mkali na kuzidi kumpa ahadi za leo kesho ambazo zilizidi kumnyima raha Onesta.

Onesta aliendelea kusubiri lakini siku chache baadae Onesta aliambiwa ukweli na mama yake mdogo kwamba hataweza kumpeleka shule kwa kuwa alikuwa hana fedha ya kutosha na kumtaka Onesta asaidie kwenye biashara ya mama nitilie (kuuza chakula) ili ipatikane fedha ya kwenda shule.

Msichana huyo alisema kwamba,licha ya kushiriki kwenye shughuli za mama nitile kwa muda mrefu bado mama yake mdogo aliendelea kushikiria msimamo wake hule hule wa kutompeleka shule kwa kisingizio cha kutokuwa na fedha za kutosha.

"Bado mama mdogo alikuwa haonyeshi msimamo juu ya suala langu la shule na aliendelea kuwa mkali tu pale nilipomuuliza", alielezea msichana huyo.

"Hadi kufikia hatua hii nilikata tamaa ya kwenda shule kabisa na moyo wangu ulikufa ganzi na nikaamua basi nijikite na biashara ya mama nitilie tu ili niweze kujikimu kimaisha. Ni muda mrefu sasa tangu nianze kuifanya biashara hii na sasa nimeshaizoea", Onesta aliongezea.

Mwandishi wetu alipojaribu kumtafuta mama mdogo wa Onesta ili kufahaumu kwa upande wake yeye anasemaje alikataa kuzungumzia chachote juu ya ili.