Wednesday 17 August 2016

Ndoa ya Masanja yaingia doa, asakwa na polisi akituhumiwa kumiliki sare za polisi

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linamsaka Emmanuel Mgaya maarufu kama, Masanja Mkandamizaji ambaye ni msanii wa vichekesho wa kundi la Orijino Komedi kwa tuhuma za kumiliki sare za jeshi hilo jambo ambalo ni kinyume na sheria, anaandika Pendo Omary.

Wakati Masanja akisakwa, tayari wasanii wenzake akiwemo, Lucas Lazaro (Joti), Serious David na Alex John wanashikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano baada ya kuonekana katika mkanda wa video wakiwa wamevaa sare zinazodhaniwa kuwa ni za jeshi hilo.

Hezron Gyimbi Naibu Kamishina wa Polisi na Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, amewambia wanahabari kuwa, wasanii hao walikamatwa Jana (juzi) saa 10 jioni.

“Walikamatwa kwa kosa la kuvaa sare zinazodhaniwa kuwa ni za Polisi ambazo ni kofia, suruali, shati, mkanda, filimbi na beji yenye cheo cha Polisi.

“Lengo letu ni kutaka kujua, walizipata wapi sare hizo na kuangalia uhalali wa kuwa nazo pamoja na kuchunguza kama hawana vifaa vingine vya Polisi tofauti na hivi walivyokamatwa navyo,” amesema Gyimbi huku akiongeza kuwa;

“Dhamana ya watuhumiwa hao ipo wazi iwapo watatimiza masharti huku upelelezi ukiendelea na watakapohitajika kwa ajili ya hatua nyingine wataitwa,”.

Wasanii hao walionekana katika video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii mwishoni mwa wiki iliyopita, wakiwa wamevalia sare zinazodhaniwa kuwa, ni za Jeshi la Polisi katika harusi ya Masanja.

Jambo lililoibua mijadala kuhusu uhalali wa sare hizo kutumiwa kiholela.

Mwanahalisi