Leo Novemba 19 katika kikao cha Bunge Dodoma Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia January Makamba amewasilisha sheria kadhaa zitakazotumika kuzuia wizi wa mitandaoni.
Alisema kuwa katika kipindi cha mwezi wa kwanza mwaka 2012 hadi Septemba 2014 jumla ya matukio 999 ya makosa mbalimbali ya kimtandao yaliripotiwa katika vituo vya Polisi hapa nchini kwa mchanganuo ufuatao; mwaka 2012 kulikuwa na makosa 414, mwaka 2013 kulikuwa na makosa 333 na mwaka huu (2014) mpaka sasa kuna makosa 252.
Alisema kuwa jumla ya kesi 212 zenye watuhumiwa 132 zilifikishwa Mahakamani na kesi 787 ziko katika hatua mbalimbali za upelelezi.
“Kwa lengo la kuongeza usalama wa matumizi ya huduma za kimtandao Wizara imekamilisha miswada mitatu ya sheria za usalama mtandaoni, Cyber Security Laws ambazo ni sheria ya kwanza, sheria ya kulinda taarifa binafsi, inaitwa Personal Data Protection.
"Ya pili ni sheria ya miamala ya kielektroniki, yaani Electronic Transaction Bill na ya tatu ni sheria ya kudhibiti uhalifu wa mtandao wa kompyuta kwa maana Computer and Cyber Crime Act. Sheria hizi tumeshazipeleka kwenye Cabinet Secretariet na zitaletwa hapa
Bungeni mwaka uja,” alisema Makamba.