MSANII wa muziki wa hip hop nchini, Ibrahimu Mussa ‘Roma Mkatoliki’ amesema hajawahi kufikiria kama atakuja kuwa mwanasiasa katika maisha
yake ingawa kuna baadhi ya viongozi na wadau mbalimbali wamekuwa wakimtaka agombee ubunge.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Roma alisema ameishapokea maoni kutoka kwa viongozi mbalimbali wakimshawishi agombee nafasi ya kisiasa ila alikataa kwa kuwa anatambua nafasi yake ni ipi katika jamii.
“Toka miaka mitano iliyopita nimekuwa nikiendelea kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wasanii wenzangu, wananchi
wa kawaida na viongozi wa dini, serikali, mawaziri na wabunge wamekuwa wakinifuata na kuniambia nigombee ubunge lakini mimi sipo tayari,” alisema.
Alisema, hajawahi kufikiria kuingia
katika siasa, anapenda asimame kama msanii, kwa sababu anaamini jukwaa ambalo analo ni bora kuliko ambalo wanasimama wanasiasa.
“Mahubiri yangu ninavyohutubia katika muziki inawezekana yana nguvu kubwa kuliko hata kiongozi ama mbunge wa jimbo fulani, kwa hiyo nafasi ambayo nipo naiona ni nzuri na sijawahi kufikiria kuingia katika siasa,” alisema.