Ripoti iliyosubiriwa kwa hamu kuhusu ufisadi nchini Afrika Kusini, imemkosoa vikali Rais Jacob Zuma kwa kujinufaisha na pesa
zilizotumiwa kuikarabati nyumba yake binfasi katika mkoa wa Kwazulu Natal.
Ukarabati huo uligharibu dola milioni 23.
Katika ripoti yake , mdhibiti wa mali ya umma nchini humo,Thuli Madonsela, amesema kuwa Zuma alikiuka sheria za maadili na kujifaidisha na pesa za Umma.
Inaelezwa kuwa, Zuma alisisitiza ukarabati huo ufanywe.
Hata hivyo, ripoti hiyo ilisema kuwa
hakudanganya wabunge kuhusu kashfa hiyo.
Lakini wito umetolewa kuwa Zuma arejeshe sehemu ya pesa hizo ambazo hazikutumika kwa ajili ya usalama wake au vinginevyo.
Vyombo vya habari nchini humo vinadai kuwa baadhi ya pesa za umma zilitumiwa katika kufadhili mahitaji ya kifahari ya bwana Zuma
kama bwawa la kuogelea na chumba cha sinema.
Taarifa kutoka nchini humo zinasema kuwa, ripoti hiyo itaathiri sana sifa ya Zuma na chama tawala ANC, huku akijiandaa kwa
uchaguzi mkuu katika kipindi cha wiki sita.