Mwanafunzi wa darasa la tatu Shule ya Msingi Majengo, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga amelazwa katika Hospitali ya wilaya
baada ya kunusurika kifo kutokana na jaribio la kuchinjwa na baba yake mzazi.
Tukio hilo lilitokea siku 10 baada ya mtu mmoja, Ustadh Mohamed Kurangwa (36), kumuua mwanafunzi wa Shule ya Msingi
Nzasa, Jamal Salum (12) kisha naye kuuawa, Mbagala, Dar es Salaam.
Kurangwa alimuua Jamal nyumbani kwake Mbagala Charambe Mianzini kwa kumchinja na kuweka kichwa cha marehemu kwenye miguu ya mtoto huyo, kisha kuupeleka mwili wake
choo cha nyumba anayoishi muuaji.
Katika tukio la Kahama, Mganga
Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Joseph Fwoma alimtaja mwanafunzi huyo kuwa ni Said Siraji (13) na alifikishwa hospitalini hapo jana alfajiri baada ya kuokotwa na wasamaria mwema
akivuja damu shingoni.
Dk Fwoma alisema baada ya kufikishwa hospitalini, madaktari walimfanyia upasuaji na
kumshona sehemu ya koromeo aliyokatwa na hadi jana alasiri hali yakeilikuwa inaendelea vizuri baada ya kuongezwa damu.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Mariamu Idd (35) alisema mwanaye alichukuliwa na baba yake mzazi, Siraji Salvatory (45) juzi na kwenda naye nyumbani kwake Mtaa wa Majengo kwa kuwa walitengana siku nyingi.
Hata hivyo, jana asubuhi alipigiwa simu kuelezwa taarifa za mtoto wake kunusurika kuchinjwa na baba yake mzazi ambaye baada
ya tukio hilo alijisalimisha polisi anakoshikiliwa hadi sasa.
Mariamu alisema mzazi huyo mwenziwe alikuwa akimchukua mara kwa mara na kwenda naye nyumbani kwake Malunga na baadaye kumrudisha akidai kuchoshwa na huduma za matibabu kutokana na mtoto huyo kuwa na matatizo ya kiafya mara kwa mara.
Polisi wilayani Kahama wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa wanafanya
uchunguzi na wakati wowote watamfikisha mahakamani baba mzazi wa mtoto huyo.