Jeshi la Polisi Mkoani Ruvuma linamhoji mtoto mwenye umri wa miaka mitatu mkazi wa kijiji cha Kondowe katika kata ya Liuli, wilaya ya Nyasa kwa tuhuma za kumpiga kichwani na fimbo mtoto
mwenzake mwenye umri wa miaka miwili na kumsababishia kifo.
Akizungumzia tukio hilo jana,
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Deusdediti Nsimeki alisema tukio hilo lilitokea
Machi 3 mwaka huu, majira ya mchana, katika kijiji cha Kondowe.
Alisema inadaiwa siku hiyo kabla ya tukio marehemu na mwenzake anayetuhumiwa kusababisha kifo chake walikuwa wakicheza jirani
na nyumba za wazazi wao.
Alieleza kuwa, Februari 27 mwaka huu majira ya saa za mchana, watoto hao wakiwa wanacheza
mtoto huyo alijeruhiwa na mwenzake kwa kupigwa kichwani kwa kutumia fimbo.
Alisema mtoto huyo baada ya kupigwa na mwenzake wazazi wake walichukulia kuwa ni
jambo la kawaida kwani watoto walikuwa wanacheza hivyo hawakutoa taarifa kituo cha
polisi kuhusiana na tukio hilo.
Alisema hata hivyo ghafla hali ya mtoto ilipoanza kubadilika ndipo wazazi wake waliamua kwenda
kituo kidogo cha polisi cha Liuli kutoa taarifa ya tukio hilo na ilipofika Machi tatu mwaka huu
majira ya saa za mchana mtoto huyo alifariki dunia.
Kamanda Nsimeki alisema polisi inaendelea kufanya uchunguzi zaidi kwa kumhoji mtoto
anayedaiwa kufanya kitendo hicho, lakini alifafanua kuwa kutokana umri mdogo wa mtuhumiwa sheria ya makosa ya jinai chini ya
umri wa miaka kumi (10) hawezi chukuliwa hatua zozote za makosa ya jinai na kwamba taratibu
zinaendelea kufanyiwa kazi ili kumaliza tatizo hilo.
Chanzo: Nipashe.