Waendesha pikipiki za abiria maarufu kama bodaboda mkoani Shinyanga, wamepewa kazi ya kuhamasisha wanaume kujitokeza
kwa ajili ya kufanyiwa tohara.
Mpango huo ulizinduliwa juzi mjini Kahama ambako zaidi ya waendesha pikipiki 300 walipewa mafunzo juu ya umuhimu wa
tohara kwa wanaume.
Mafunzo hayo yalitolewa na Shirika la IntraHealth International kwa kushirikiana na Kamati ya uendeshaji ya afya ya mkoa wa
Shinyanga na Wilaya ya Kahama na polisi kitengo cha usalama barabarani.
Hatua hiyo imeelezwa kutoa msukumo mpya kwa wanaume wakazi wa Shinyanga katika suala zima la tohara kwa lengo la
kuzuia maambukizi ya Ukimwi.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka kwa Mratibu wa Ukimwi wa Mkoa wa Shinyanga, Dk Mawazo Amri, wanaume 71,031 wamefanyiwa
tohara wilayani Kahama kati ya mwaka 2009 na 2013, ikiwa ni zaidi ya nusu ya lengo la wanaume 142,727.
Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa inayotajwa kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya Ukimwi kwa asilimia 7.4 zaidi ya kiwango cha kitaifa ambacho ni
asilimia 5.1.