Mkali wa filamu nchini, Baby Madaha, amewataka wasanii kubadilika kwa kuacha kutunga sinema za mapenzi badala yake wajikite kwenye zile zinazozungumzia matatizo
yanayoizunguka jamii nchini kama uuzaji wa dawa za kulevya.
Akizungumza jana, Madaha alisema kuwa, amefurahishwa na
ujio wa kampuni ya 5 Effects Movies Ltd, ambayo imeonekana kusimamia katika utoaji wa filamu zinazozungumzia jamii zaidi badala ya mapenzi, ikiwamo kazi
yao ya Mr. Kadamanja, inayopiga vita biashara ya dawa za kulevya.
“Kumekuwa na kawaida ya wasanii
wengi wa Tanzania, kucheza sinema za mapenzi kwa kujua kuwa ndizo zinawatoa zaidi bila kujua kama hata zinazozungumzia masuala ya jamii zinaweza kufanya vizuri. Tujifunze kwa 5 Effects Movies Ltd ambayo kwa asilimia kubwa imekuwa ikitengeneza
muvi zinazozungumzia matatizo ya
jamii,” alisema Madaha.
Msanii huyo aliongeza kuwa,
amefanikiwa kuona filamu ya Mr.
Kadamanja ambayo imechezwa na Adam Kuambiana, ikiwa katika hatua za mwisho kukamilishwa na kuona umuhimu wa kuwa anacheza sinema za aina hiyo, ili kutoa elimu ya kupiga vita
dawa hizo, ambazo zimekuwa zikivunja nguvu kazi ya taifa, kwani watumiani wengi ni vijana.
Filamu ya Mr. Kadamanja inatarajiwa kuingizwa sokoni mwishoni mwa mwezi huu na imechezwa na wasanii wakongwe
na chipukizi kama Adam Kuambiana, Stanley Msungu, Steven Almasi ‘Dk. Almasi’ na Miriam Ismail.