Ilikuwa kama muda wa
saa mbili usiku nilipokatiza maeneo yao wanapojibanza ukutani wakisaka tonge na
vijisenti kwa mahitaji mengine muhimu.
Nilipotokeza kwenye
uchochoro ambapo huwa wanajipanga kusubiria wateja walianza kunivamia huku kila
mmoja akijinadi kuwa mzuri zaidi ya mwenzie.
Nikiwa nimeshikwa na
kigugumizi kilichofungamana na uwoga nilikosa cha kusema huku nikiwa nakodolea
macho kwenye nyuso zao.
Kunipotezea ndilo jambo
lililofuatia baada ya kugundua kuwa sikua mteja wao. Walinipotezea huku wakiambiana
kuwa achana nae huyo hana lolote.
Kitendo cha
kupotezewa kukawa ndio kupona kwangu. Daaa! Nikaendelea na safari yangu
kuelekea barabarani huku kijasho chembamba kikinitoka.
Niligeuza shingo
na kutazama nilikotoka. Macho yangu yakakutana na bango lililoandikwa Kimboka
bar, nikajiwa na kumbukumbu kwamba nilishawahi kuambiwa kuwa eneo hilo lina
wanawake wanaouza miili.
Kumbe ndio hapa!
Nilijiambia mwenyewe. Lakini kilichoniumiza ni nyuso za akina dada
nilizozikodolea. Nyuso zilizojaa mengi ya kuzungumzia. Nyuso ambazo zinajieleza
kwa kuziangalia tu.
Nyuso zao tu
zilikuwa kipimo tosha cha kupima umri wao. Maskini, ni wasichana wadogo ambao
kwa kuangalia nyuso zao ni wa juzi tu.
Yaani wengi wao
ni chini ya umri wa miaka 18, umri ambao bado ni wa mtoto wa shule aliyetakiwa
kuwa nyumbani mezani akijisomea alichofundishwa na mwalimu wake.
Ni hatari sana
kwa maisha yao na kizazi kijacho. Siwezi kujua sababu iliyowafanya wajiingize kwenye
biashara hile lakini haijalishi nini kimewatumbukiza, ni hatari sana kwao na
kwa taifa kwa kuwa nguvu kazi inaangamia.