Wednesday, 26 March 2014

Ukiachana na kutakwa kimapenzi, je, wafanyakazi wa ndani wana matatizo gani mengine? Twende hapa na vitendo ukafahamu zaidi.

Ukiachana na kutakwa kimapenzi, je, ulishawahi kujiuliza ni changamoto gani nyingine wanazozipata wanawake/wasichana wanaofanya kazi za ndani?

Wanawake/wasichana mbalimbali wanaofanya kazi za ndani waliielezea kazi hiyo ya ndani kama kazi yenye changamoto nyingi sana ambazo upelekea kazi hiyo kuchukuliwa kuwa ngumu.

Wafanyakazi mbalmbali walitoa yao ya moyoni walipokuwa wakihojiwa na mtangazaji wa kituo fulani cha redio juu ya changamoto wanazozipata kwenye kazi yao.

Mazingira magumu ya kazi ni changamoto iliyoelezewa kwa hisia kubwa sana. Walieleza ugumu wanaoupata ni kama vile, kutopata chakula ndani ya muda, kutupiwa maneno machafu na matajiri wao yanayoambatana na matusi na kashfa jambo linakomfanya mfanyakazi asiifurahie kazi yake.

Kutolipwa mshahala wao ndani ya muda unaotakiwa ni tatizo kubwa linalowatatiza wafanyakazi wa ndani. Walisema kuwa matajiri wengi wanashindwa kulipa mshahala panapo muda husika na hata kama wanaamua kulipa hawalipi kiasi chote jambo linalowasababishia ongezeko la ugumu wa maisha.

Kutoajiriwa ni jambo ambalo wafanyakazi hao wa ndani wanalia nalo kila kukicha, ni wajibu wa mtu anayefanyiwa kazi kumwajiri mfanyakazi wake wa ndani ili kumtimizia haki yake ya msingi ya kutambulika kama muajiriwa.

Pia walilalamikia suala la kutokuwepo kwa mikataba ya kazi itakaelezea sheria za kazi husika ila wafanyakazi hao walisema pindi wanapoulizia kuhusu mikataba wanaishia kuambiwa kama wanataka wafanye kama hawataki waache kazi.