Mfanyakazi wa Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa cha mkoani Morogoro, Adam Danford amekamatwa mkoani hamo, akituhumiwa kusafirisha vijana 55 kutoka wilayani Kibondo kwenda kufanya kazi kwenye mashamba ya miwa.
Polisi Mkoa wa Kigoma, ilimkamata
ikimtuhumu kujihusisha na biashara haramu ya kusafirisha binadamu, waliokuwa wakisafirishwa kwenye basi la Lushanga.
Anadaiwa kukutwa akisafirisha vijana hao wakiwemo watoto, kutoka vijiji vya Lugunga na Kitahana wilayani Kibondo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kibondo, Venance Mwamoto ambaye ni Mkuu wa Wilaya, aliwaambia
waandishi wa habari kwamba vijana husika
pia wanashikiliwa katika kituo kikuu cha Polisi wilayani Kibondo kwa mahojiano zaidi.
Mwamoto alisema wanamtuhumu mtu huyo kwa kufanya biashara ya usafirishaji wa binadamu, kusafirisha watoto chini ya miaka 18 kwenda kufanya kazi ngumu katika mazingira hatarishi bila ulinzi wa wazazi wao ambavyo ni kosa kisheria.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema polisi walipata habari kutoka kwa raia wema hivyo kuweka mtego na kukamata basi hilo la Lushanga, lililokuwa limebeba watoto hao.
Alisema ilihofiwa kuwa miongoni mwa watoto hao, kunaweza kuwepo raia kutoka nchi jirani, kutokana na vijiji wanakotoka
vijana hao, vinapakana na Burundi.
Katibu Tawala wa Mkoa Kigoma, John Ndunguru aliamuru pia kukamatwa kwa viongozi wa vijiji vya Lugunga na Kitahana wilayani Kibondo, ambako watoto hao
wanatoka.
Akizungumza katika mkutano huo na waandishi wa habari baada ya kutembelea kituo cha Polisi Kibondo na kufanya mahojiano mafupi na watoto hao, Ndunguru
alisema viongozi wahojiwe kuhusu tukio hilo.
Aliagiza wahojiwe juu ya uhusika wao kuhusu kukusanya watoto na kutoa vibali kwa mawakala, waliotumwa kufanya kazi hiyo
kwa kuwapa barua kuidhinisha kuwa jambo hilo ni halali, wakati ni kosa kisheria.
Alisema kuwa kitendo cha kuchukuliwa kwa watoto hao na kwenda kufanyishwa kazi nje
ya mkoa huo, kinapunguza nguvu kazi ya mkoa, hasa wakati huu ambao Serikali imeanza utekelezaji wa mkakati wa kuimarisha kilimo kwa kupanua mashamba.
Mtuhumiwa huyo, Danford, alijitetea, kwamba alifanya kazi hiyo baada ya kupewa idhini ya kufanya hivyo na uongozi wa
Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa, akiwa na barua kwenda kwa viongozi wa vijiji.
Alidai kuwa barua hiyo, ilieleza aina ya watu wanaotakiwa na malipo kwa ajili ya kazi hiyo huku akidai hakuona kosa kufanya kazi hiyo, kutokana na kupata idhini kutoka kwa viongozi wa vijiji na kata, ambao licha ya kumsaidia kukusanya vijana hao, walimpatia
barua za kumsaidia atakapokamatwa, zikionesha kuwa viongozi hao wa vijiji, wamebariki mpango huo.
Mmoja wa vijana hao, Damas Josephat alidai walivutiwa kujiunga na safari hiyo kwenda kufanya kazi Kiwanda cha Miwa Mtibwa,
kutokana na malipo ya Sh 750,000
waliyoahidiwa wangelipwa kwa mwaka kwa kazi hiyo huku gharama za kuishi na matibabu, zikiwa juu ya kiwanda hicho.
Alipoulizwa, Meneja wa Kiwanda cha Mtibwa, Hamadi Yahaya, alikiri Danford kuwa mwajiriwa wao, aliyetumwa na kampuni kwenda kutafuta watu wa kufanya
kazi katika mashamba yao.
“Tumekuwa tukitafuta vibarua kutoka Kigoma na Iringa na maeneo mengine, lakini
tumekuwa tukifanya kazi hii kwa kushirikiana na serikali za vijiji. Msimu huu tumemtuma mfanyakazi wetu, lakini inaonekana kuwa viongozi wa vijiji wametupatia vijana ambao
wako chini ya umri,” alisema.
Alisema baada ya kutokea tatizo hilo, kuanzia sasa watakuwa wakifanya kazi hiyo kupitia ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
“Tumezungumza na Mkuu wa Wilaya Mwamoto, kwa sasa barua zetu zitakuwa zikipitia kwake kuandika nakala kwa Mkuu
wa Mkoa. Kwa sasa tumeshaandika barua mpya, ili kupata vijana wanaotakiwa na wale wenye umri mdogo tutawaacha,” alisema.
Yahaya alisema makubaliano yao na serikali za vijiji ni kwamba kila mfanyakazi, ambaye kiwanda kingemtumia kwa ajili ya palizi kwa
miezi sita, angelipwa Sh 3,000 kwa siku,huku kiwanda kikigharimia chakula, na malazi kwa muda wote huo.