Mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi hautatatuliwa kisheria,badala yake itakuwa kijamii kwa kuhoji wananchi wa
pande husika. Mgogoro huo unahusu mpaka katika Ziwa Nyasa.ambao sasa wananchi wa kila upande, watahojiwa juu ya madhara wanayodhani watapata kutokana na mpaka kuwa ndani ya ziwa hilo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu wizara yake.
Alisema uamuzi ulifikiwa katika kikao kilichoshirikisha pande zote, mbele ya jopo la wazee watatu wenye busara wanaoshughulikia mgogoro huo ambao ni Rais mstaafu wa Msumbiji, Joachim
Chissano, Rais mstaafu wa Afrika Kusini,.Thabo Mbeki na Rais mstaafu wa Botswana, Festus Mogae.
Alisema katika kikao hicho, baada ya pande zote kusikilizwa na kuulizwa maswali ya ana.kwa ana mjini Maputo Msumbiji, pia
waliulizwa iwapo wana lengo la kupeleka suala hilo katika Mahakama ya Kimataifa.
Membe alisema wote walisema wana imani na jopo hilo hivyo wakashauri kuacha kulishughulikia kisheria na kuanza kijamii kwa kwenda kwa wananchi na kuwauliza madhara ya kila upande ikikubaliana na nyingine.
Membe alisema katika suala la kijamii asilimia 60 ya maji yanatoka katika mito ya Tanzania na kuingia katika Ziwa Nyasa huku
mto mmoja ukitoa maji katika ziwa hilo.
Pia katika ziwa hilo kilometa 10 za ardhi zimesombwa katika ziwa hilo hivyo yako makaburi ya jamii mbalimbali za kitanzania.
Alisema kikao kinachofuata kitakuwa Juni mwaka huu kuangalia matokeo ya mahojiano
hayo kutokana na kwamba Mei nchi ya Malawi itafanya uchaguzi na siyo vema kufanya kikao sasa.
Alisema katika kikao hicho cha pili
kitaendelea na mikutano mingine kadhaa itakayofanywa na upande utakaoshinda katika uchaguzi huo wa Malawi kutokana na kuwa suala hilo lina hisia za kisiasa.
Wakati huo huo, akizungumzia mgogoro wa Rwanda, alisema kinachotakiwa ni kuaminiana baina ya Tanzania na Rwanda
kwani hakuna mgogoro wa nchi hizo mbili isipokuwa ni maneno ya kusikia.
Alisema ili kuaminiana ni vema kutumia vyombo vya usalama kuchunguza na kupata uhakika kabla ya kuanza kushutumiana.
Pia alisema Tanzania iko katika maandalizi ya mwisho kupeleka Kikosi Maalumu cha kulinda amani Sudan Kusini kama ilivyokuwa
kwa DRC, jambo ambalo majeshi hayo yatafanya kazi chini ya Baraza la Umoja wa Mataifa.
Hatua hiyo imetokana na maombi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kwa
nia ya kuleta amani kutokana na kazi nzuri zilizofanywa katika nchi nyingine.