Tuesday 2 August 2016

Hofu yatanda baada ya fisi kumng'ata mtoto makalio

Wakazi wa kitongoji cha Minjaleni kata ya Mpapura mkoani Mtwara wameiomba Serikali kumthibiti fisi anayezunguka kwenye kata hiyo, baada ya kumjeruhi vibaya kwa kumg’ata kwenye makalio, mtoto wa miaka 8 Astara Hamis mwanafunzi wa darasa la 1, na pia kuua mbuzi 20 katika kipindi kisichozidi miezi 2.

Mwenyekiti wa kitongoji hicho Issa Mshamu amesema kufuatia kutokea ghafla kwa fisi huyo anayezunguka nakujeruhi, wananchi wamekuwa na hofukubwa na kushindwa kufanya shughuliza maendeleo ikiwemo kwenda kuvuna mtama mashambani, ikizingatiwa huu ni wakati wake wa uvunaji wa zao hilo.

Kwa upande wake, mama mzazi wa mtoto Astara Hamisi Bibi Fatuma Mataka amesema mwanae alishambuliwa na fisi majira ya saa 12.30 jioni alipokwenda na watoto wenzake mto  mambi kuoga, lakini aliokolewa na wananchi wakati fisi huyo akimburuzia mtoto huyo porini.

Alipoulizwa juu ya hali hiyo, diwani wakata ya Mpapura Maupa Bakari amekiri kuwepo kwa tishio kubwa la fisi kwenye kata hiyo na kumjeruhi vibaya na fisi kwa mtoto Astara, na hivyo amesema,mbali na tukio hilo kufikishwa kwa viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Mtwara, mipango anaifanya yeye kama diwani ya kumtega fisi huyo kwa nyavu.

Itvhabari