Saturday, 28 May 2016

Wema aweka wazi kuwa amewahi kutoa ujauzito, utumizi wa mitishamba ili ashike ujauzito tena

“OOOH nalia miye, nalia mgumba sina mwana, baba Mungu nalia miye, nalia mgumba sina mwana,” ni baadhi ya maneno yaliyoimbwa na Bendi ya African Revulation ‘TamTam’ ukiwa ni utunzi wa Mwanamuziki Muumini Mwinjuma ‘Kocha wa Dunia’ miaka kadhaa iliyopita.

Ujumbe uliomo kwenye wimbo huo unaelezea kilio cha mwanamke anayesakamwa katika jamii kwa kushindwa kupata mtoto.

Maneno ya wimbo huo ni kisu kikali ndani ya moyo wa staa wa filamu za Kibongo, Wema Isaac Sepetu.

Wema amekuwa akiumizwa na mashabiki wake pale anapoposti picha za watoto katika mitandao ya kijamii.

“Binafsi nawapenda sana watoto, hivyo najihisi kuwa huru kuposti picha zao, lakini mashabiki hawanielewi, huwa wananiita mgumba, tasa na maneno kama hayo yakuniudhi.

Wakati mwingine wananitumia ujumbe na kuniambia: ‘Zaa wa kwako’, au ‘Utaishia kuposti picha za watoto wa wenzako.’

“Binafsi huwa ninaumia sana, kwa kuwa sina moyo wa chuma,” anasema staa huyo ambaye ni maarufu kwa jina la Madam na kudai kuwa ulifikia wakati alikuwa akijifungia chumbani na kumwaga machozi.

“Nililia sana, sikuwa napenda watu wajue, nilijifungia chumbani na kulia, nilipotoka nje watu hawakujua kama nilikuwa nalia na kwa kiasi gani naumizwa na maneno hayo,” anafunguka Wema alipofanya mahojiano na mwandishi wa makala haya.

Nawaza kama Wema ameshawahi kutoa ujauzito?

Wema wala hafichi, katika maisha yake ya uhusiano anakiri wazi kwamba amewahi kupata ujauzito wa staa wa zamani wa filamu marehemu, Steven Kanumba lakini aliutoa.

“Nilikuwa sifikirii kuhusu mtoto kipindi hicho. Nilikuwa na miaka 18, sikuwa nimejiandaa kupata mtoto na bado nilikuwa naishi kwa wazazi,” anasema.

Kutumia dawa za asili

Staa huyo wa filamu za My Vallentine, Point Of No Return na Madam anafafanua kwamba kilifika kipindi alijutia uamuzi wake huo wa kutoa ujauzito.

Miaka minne iliyopita akiwa na mchumba wake staa wa muziki wa Bongofleva, Nassibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ Wema alihaha kusaka mtoto na kufikia hata kutumia dawa za kiasili lakini hakuambulia kitu.

“Nakumbuka nilipokuwa na ex wangu, tulijitahidi sana kupata  mtoto,  nilienda kwa daktari na hata kunywa  dawa za asili lakini sikufanikiwa,” anafafanua.

Anatoka na nani sasa?

“Idris is my baby,” anasema Wema na kuachia tabasamu.

“Watu watuache na Idris, nadhani tunapendana sana pamoja na kwamba tunagombana mara kwa mara, lakini tunajuana wenyewe, watuache tu” aliongeza.

Ukweli kuhusu mimba ya Idris

Mwana Bongofleva, Nay wa Mitego amemchana Wema kwenye wimbo wa Shika Adabu Yako, akidai kwamba hakuwa na ujauzito bali alikuwa akitafutia kiki (umaarufu), je, ni kweli?

Kabla ya kujibu, Wema anavuta pumzi za kutosha, kisha anasema: “Nilikuwa  na ujamzito kweli.” Kisha anaendelea:

“Mwezi wa 12 mwaka jana, nilikuwa najihisi kuongezeka uzito, hivyo nikaenda kwa daktari kwa lengo la kusafisha kizazi.

“Nilipofika kwa dokta nilimwambia hata hivyo nimemisi period, akaniambia ya Mungu mengi pengine nime-concive, nilimkatalia katakata.”

Wema anaendelea kwamba daktari alimshauri akanunue kipimo cha ujauzito ajipime haja ndogo atakapoamka asubuhi na asile kitu chochote kwa ajili ya zoezi la kusafisha kizazi.

“Nilipokuwa narudi nyumbani nilipitia dukani na kununua kipimo hicho na asubuhi nikafanya hivyo, nilishtuka sana, nilikuwa kama nimewehuka nilipoona mistari miwili katika kipimo, siku zote nilizoea kuona mstari mmoja.

“Nikawauliza rafiki zangu nikiwa katika hali ya furaha baadaye nikampigia daktari nikamwambia nimepima lakini sielewi ninachokiona maana kuna mistari miwili, aliniambia niende na kipimo hicho na akanihakikishia kwamba nilikuwa na ujauzito.

“Sikutaka kumwamini, nikamtaka anipime, hapo ndipo nilipothibitisha, nilisema sasa watanikoma,” anasema.

Nini kilitokea?

Siku ambayo sipendi kuikumbuka ni ile niliyokwenda msalani kwa ajili ya kujisaidia haja ndogo kisha nikaona donge la damu likidondoka, nilichanganyikiwa kwa kuwa daktari aliniambia sikutakiwa kuona damu.

“Nilipompigia mama yangu naye alinilaumu sana badala ya kunipa pole aliniambia, ‘Wema nilikuambia mimba haitangazwi! Unaona sasa kilichotokea, niliyajua madhara ya kufanya hivyo!”

Wema anasema alikwenda kwa daktari akiambatana na Idris na kuthibitishiwa kuwa ni kweli  ujauzito ulikuwa umetoka na ulikuwa na wiki 13.

Angeweza kujifungua pacha

Wema anasema, daktari alimwambia ndugu yake mwingine aliyeambatana naye kwamba ujauzito huo ulikuwa ni wa watoto wawili, yaani pacha.

Mwanaspoti