Monday, 30 May 2016

Mbona kimya kimya wana jangwani, ni kweli mmelipa milioni 180 kumnasa Kipre Tchetche?

Fedha inaongea, baada ya kuifanyia Simba umafia kwa kuwasajili Hassan Ramadhan ‘Kessy’ na Juma Mahadhi sasa jeuri ya Yanga imehamia kwa Azam, baada ya kumnasa straika wa timu hiyo, Kipre Tchetche kwa dau la shilingi milioni 180.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ambazo BINGWA imezipata, zinadai kuwa Yanga tayari imemnasa Kipre kwa dau hilo la fedha na kumfunga Jangwani na mkataba wa miaka mitatu.

Inadaiwa kuwa kuondoka kwa kocha Stewart Hall katika klabu ya Azam kumewaumiza mastaa wengi wa kimataifa wa timu na ndiyo moja ya sababu kubwa za Kipre kuamua kutimkia Jangwani.

Chanzo cha habari hizi kimeliambia BINGWA kuwa mbali na kumtimua Hall, Azam pia imekuwa na mpango wa kutaka kumuondoka kwenye timu hiyo Kipre Bolou pacha wa Tchetche kitendo ambacho kilimuumiza staa huyo ambaye aliamua kutua Jangwani.

Yanga imekuwa ikifukuzia saini ya Kipre Tchetche kwa muda mrefu sasa na kati siku za karibuni inadaiwa kuwa staa huyo amekuwa akikutana kwa siri na baadhi ya viongozi wa miamba hiyo ya Jangwani.

“Unajua kwa nini Kipre hakucheza fainali ya Kombe la Shirikisho?” kilihoji chanzo cha habari hizi. “Kabla ya fainali walitakiwa wasitoke kambini, lakini yeye alitoka na kukutana na viongozi wa Yanga kwa ajili ya kujadili masuala ya usajili.”

Inadaiwa kitendo cha kutoka kambini bila ruhusu ndiyo kilisababisha asipangwe kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho ambayo Yanga ilichukua ubingwa kwa kuichapa Azam kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa.

Licha, ya viongozi wa Yanga kuonekana kufanya siri sana ishu hii ya usajili wa Kipre, lakini chanzo cha habari hizi kililiambia BINGWA kuwa siku si nyingi kutoka sasa habari hizi ambazo zinatarajiwa kulishtua Taifa zitatangazwa rasmi.

Pamoja na Yanga kudaiwa kukamilisha usajili wa Kipre, staa huyo anadaiwa kuwa bado na mkataba wa mwaka mmoja Azam na klabu yake hiyo imedai kuwa kama Yanga wanataka kumchukua basi wafuate utaratibu kwa kukaa nao mezani na kumalizana kwa sababu wao hawana nia ya kumzuia machezaji kama anataka kujiunga na timu nyingine.

BINGWA lilipojaribu kuwatafuta viongozi wa Yanga kuthibitisha usajili huu simu zao ziliita bila majibu, lakini mmoja wa vigogo ndani ya klabu hiyo aliyegoma jina lake kutajwa gazetini alimwambia mwandishi wetu awe na subira kwa sababu karibuni habari hizo zitatangazwa rasmi.

Kipre kwa sasa anadaiwa kuwa nchini kwao Ivory Coast alipoenda kwa mapumziko kabla ya kurudi kukamilisha uhamisho wake wa kutua Jangwani rasmi.

Katika hatua nyingine, Mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wanatarajia kuweka kambi ya muda mfupi nchini Afrika Kusini (Sauzi) kujiandaa na mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya MO Bejaia ya Algeria ugenini.

Yanga ambao ni wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, wanatarajia kuondoka nchini Ijumaa wiki hii kuelekea Sauzi kwa ndege ya Shirika la Afrika Kusini hii ni baada ya wachezaji kumaliza mapumziko ya wiki moja.

Akizungumza na BINGWA jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, alisema timu hiyo itarejea mapema kwa ajili ya kucheza mechi moja ya kujipima nguvu kabla ya kukutana na MO Bejaia ugenini.

“Tumechagua kuweka kambi ya muda mfupi Afrika Kusini kutokana na hali ya baridi iliyopo nchini humo ili wachezaji waweze kuizoea tutakaposafiri kwenda Algeria kuwakabili wapinzani wetu MO Bejaia,” alisema Muro.

Yanga itaanza kampeni yake ugenini dhidi ya Mo Bejaia Juni 17 kabla ya kuwa mwenyeji wa TP Mazembe Juni 28 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizia mzunguko wa kwanza nyumbani dhidi ya Medeama ya Ghana Julai 15, mwaka huu.

Bingwanewspaper