Tuesday, 29 April 2014

Jamaa akutwa amejinyonga chooni kwa kukumbuka mapenzi ya mkewe

Mkazi wa Mtoni Kijichi, Richard Kijazi ,36, amekutwa amekufa kwa kujinyonga chooni na kuacha ujumbe kwamba amejiua kwa sababu ya kumkumbuka marehemu mkewe. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo, alisema jana kuwa Kijazi alijiua juzi saa 11:15 jioni katika maeneo ya Mtoni Kijichi, Wilaya ya Temeke.

Alisema Kijazi alikutwa amejinyonga kwa kutumia kitambaa cha nguo alichokitundika kwenye kenchi ya choo ya nyumba anayoishi. Ujumbe uliokutwa katika eneo hilo ulisomeka:

“Hajahusika mtu yeyote kuhusu hili, nimemmiss Mama John wangu, nizikwe Dar es Salaam na Mchungaji Haule naomba ujumbe huu uheshimiwe.”

Kwa mujibu wa Kamanda Kiondo, uchunguzi wa awali umebaini kuwa Mama John alifariki mwaka 2012 baada ya kuugua malaria na tangu wakati huo Kijazi alikuwa akijaribu kujiua na kuokolewa na ndugu zake.