Saturday, 15 February 2014

AKOLEA MOTO WAKATI ANAIGIZA MCHEZO WA KUCHEZA NA MOTO, WATAZAMAJI WADHARAU MAYOWE YA KUOMBA KUSAIDIWA WAKIJUA NI SEHEMU YA MCHEZO.

Kijana mmoja mkazi wa Yombo Vituka aliyejulikana kwa jina lake maarufu la Abdul Khan kutoka kwa rafiki yake wa karibu amefariki dunia jana katika hospitali ya  Taifa ya Muhimbili baada ya kuungua moto wakati anaigiza mazingaombwe.

Tukio hilo limetokea siku tatu zilizopita kwenye ukumbi wa Leopard Pub uliopo Yombo Vituka Dar es salaam ambamo alikwenda kufanya maonesho.

Rafiki yake wa karibu alisema kuwa, wakati anaigiza mchezo wa kucheza na moto, moto ulidaka nguo aliyokuwa amevaa na kuanza kusambaa sehemu mbalimbali za mwili.

Aliendelea kusema kuwa, wakati moto unawaka mwilini watazamaji waliokuwepo walijua ni sehemu ya mchezo ambapo waliendelea kumshangilia.

Baada ya muda alianza kulalamika maumivu  ndipo watu waliokuwepo eneo la maonesho wakagundua kuwa alikuwa anaungua na huku akiwa ameshaungua sehemu kubwa ya mwili wake.

Alichukuliwa na kukimbizwa hospitali ya wilaya ya Temeke na kushindikana kutibiwa na kupelekwa hospitali ya taifa ya Muhimbili ambako alifariki dunia.