"Vijana wengi wamekuwa na mtazamo tofauti juu ya baadhi ya kazi za kufanya kwamba kazi fulani si kazi inayostahili kufanywa na yeye kama kijana kwa sababu mbalimbali kama vile kujishusha".
Kuali hiyo ilizungumzwa na kijana anayejishughulisha na ushonaji viatu maeneo ya Yombo relini ambaye alisema kuwa, japokuwa kazi hiyo inadharaulika lakini ina faida kubwa.
Kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Yusufu Lioka alianza kujishughulisha na kazi ya ushonaji viatu miaka kadhaa iliyopita ambayo alisema imempatia mafanikio mengi.
Alisema kuwa mitazamo ya watu wengi kuhusu kazi yake mara nyingi huwa ni mitazamo hasi haswa kwa vijana wengi ambao wanaichukulia kama kazi inayodhalilisha.
Na ama kweli mitazamo hiyo inawachelewesha vijana kujikwamua kimaendeleo kwa kutoelewa hakuna kazi isiyolipa.
Moja ya mafanikio anayojivunia nayo ni kufanikiwa kujenga nyumba mbili maeneo ya Yombo vituka ambazo moja anaitumia kulala na failia yake huku nyingine alidai anaitumia kupangisha na kujipati kipato cha kila mwisho wa mwezi.
Ukiachana na nyumba mbili alizofanikiwa kujenga kupitia kazi yake ya ushonaji viatu, pia amefanikiwa kupata ardhi yenye ukubwa wa robo heka ambayo anategemea kujenga nyumba siku za hivi karibuni.
Sio hayo pekee, pia kazi yake inamwezesha kuwapeleka watoto wake shule na kuwapatia huduma zote za msingi.
Kujitengenezea heshima pia ni jambo analojivunia kwani kutokana na mafanikio yote aliyoyapata jamii inamchukulia kama mfano wa kuigwa.
Ni mafanikio ambayo kwa hali ya kawaida ni vigumu kuamini lakini hakuna kisichowezekana na hakuna kazi isiyolipa ila kinachohitajika ni umakini tu.