Ni nadra sana kukutana na shule ya chekechea inayotoa nafasi kadhaa za masomo kwa watoto yatima pamoja na watoto wa mitaani ambao wamahitaji msaada wa hali ya juu hasa wa kielimu kama ilivyofanya shule ya chekechea ya S.t Neema.
Shule ya S.t Neema English Medium Nursary school iliyopo Yombo relini jijini Dar es salaam inaendesha programu ya kuwasaidia watoto yatima kwa kutoa nafasi tano za masomo kwa watoto hao kila mwaka wa masomo.
Akizungumzia zoezi hilo, mwalimu mkuu msaidizi Isaack Ngalawa amesema kwamba, wameamua kuendesha zoezi hilo ili kukabiliana na tatizo la ongezeko kubwa la watoto yatima na watoto wa mitaani linaloendelea kuielemea jamii.
"Uongozi wa shule yetu imeamua kuendesha zoezi hili ili kujaribu kupunguza tatizo la watoto yatima na wa mtaani ambao ni tatizo kubwa kwa sasa katika nchi yetu", Ngalawa alisema.
Pia Ngalawa aliongezea kwa kusema kwamba, wameamua kuendesha zoezi hilo ili kushirikiana na serikali kwenye kampeni ya kupambana na ongezeko la watoto yatima na watoto wa mitaani.
Ngalawa alisema, tangu nafasi hizo zitangazwe mwitikio wa wazazi umekuwa mkubwa ukilinganisha na idadi ya nafasi zilizotangazwa na uongozi wa shule kwa kuwa kuna idadi kubwa ya watoto yatima (walio katika mazingira magumu).
"Tulianza kutanangaza nafasi tatu kila mwaka,tukaona haja ya kuongeza,tukaongeza hadi tano lakini bado nafasi hizo zinaonekana chache kutokana na idadi ya watoto wenyewe kuwa nyingi", alielezea mwalimu mkuu msaidizi.
Ongezeko la watoto yatima nchini imezidi kushika kasi licha ya kampeni mbalimbali zinazofanyika na setikali na taasisi binafsi kupunguza na kutokomeza suala la watoto yatima.