Monday, 23 November 2015

Sina uwakika kama wasomi hao wa Jimboni Ruangwa walioelezea mambo aliyoyafanya Mbunge Majaliwa jimboni kwake ni wakazi wa jimboni humo; na sina uwakika kama wasomi hao waliomsifia Mbunge majaliwa wanaijua hali halisi ya maendeleo ya jimboni humo; na sidhani kama wananchi hawa waliogoma kuitikia salamu yake wakati wa kampeni ndio hao waliompa misifa lukuki!

Gazeti la Habari Leo la Novemba 22, 2015 limechapisha taarifa inayowahusu wasomi kadhaa na wananchi wa wilayani Ruangwa jimbo ambalo Kassim Majaliwa, mbunge wa jimbo hilo na Waziri Mkuu wa Tanzania wakimmwagia sifa lukuki Mbunge huyo.

Wasomi hao kutoka jimboni Ruangwa ambamo Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa anatokea ambao hawakutajwa majina yao wameelezea namna wanavyomwelewa Mbunge huyo na kuelezea mambo kadhaa ambayo ameyafanya jimboni humo ndani ya kipindi cha miaka 5 iliyopita.

Moja ya mambo yaliyoainishwa na wasomi hao ambao hawakutajwa majina yao bila kueleza sababu ya kutowataja ni suala la elimu ambapo wamedai kuwa Mbunge majaliwa katika kipindi cha miaka mitano ya ubunge amesaidia sekta ya elimu kwa mapana.

Lakini licha ya kumsifia Mbunge huyo kuwa amesaidia vya kutosha kwenye eneo la elimu; lakini ukweli ni kwamba bado kuna changamoto ambazo zinaumiza eneo la elimu jimboni Ruangwa ambako Waziri Majaliwa anatokea.

Changamoto hiyo ni ya wanafunzi wa shule za msingi kutojua kuandika na kusoma kama inavyotakiwa, tatizo linalosababshwa na misingi mibovu waliyonayo wanafunzi hao. Ni tatizo ambalo lilihitaji ufumbuzi, na si kwa kujenga maabara na kusambaza vitabu kama wasomi hao walivyoelezea kwenye taarifa iliyoandikwa kwenye gazeti la Habari Leo.

Sina uwakika kama wasomi hao wa Jimboni Ruangwa walioelezea mambo aliyoyafanya Mbunge Majaliwa jimboni kwake ni  wakazi wa jimboni humo. Na sina uwakika kama wasomi hao waliomsifia Mbunge majaliwa wanaijua hali halisi ya maendeleo ya jimboni humo.

Bila shaka watakuwa hawaelewi chochote kuhusu jimbo la Ruangwa, na kama wanaelewa basi watakuwa wamelishwa unga wa ndele ili wakose uwezo wa kuelezea ualisia uliomo ndani ya jimbo.

Katika taarifa hiyo ya Gazeti la Habari Leo, wananchi jimboni Ruangwa nao wametajwa kuwa miongoni mwa wanaomwelezea Mbunge Majaliwa kuwa ni Mbunge aliyeyafanya mengi jimboni kwake.

Kama nitakuwa nakumbuka vilivyo kipindi cha kampeni wananchi hawa hawa wa Jimbo lake ndio waliokuwa wanagoma kumwitikilia salamu aliyokuwa akiitoa kwenye mikutano yake kwa sababu ya kutotatua matatizo yao muhimu, sasa iweje leo wananchi hawa waseme hakuna kama Majaliwa na kummwagia matilioni ya sifa.

Lakini hii yaweza kuwa kama ile ya wasomi ambao hawakutajwa majina bila sababu ya msingi kwa nini hawakutajwa.

Wananchi hawa wanaoangaika kutafuta maji kila kukicha na kuambulia kutumia maji yenye tope katika shughuli zao za kila siku, sidhani kama wanaweza kufungua vinywa vyao na kuanza kusema hakuna kama Mbunge Majaliwa, na, kama yupo basi atakuwa amerogwa.

Wananchi hawa wanaoamua kununua dawa maduka binafsi ya dawa na kumeza bila kujua nini haswa kinachowasumbua kwa sababu wanakosa vipimo hospitali, sidhani kama wananchi hao wanaweza kufungua vinywa vyao na kumsifia Majaliwa.

Vijiji vingi vinavyotengeneza jimbo la Mbunge na Waziri Mkuu Majaliwa vinakabiliwa na kiu kubwa ya maji. Siwezi sema kiu ya maji safi kwa sababu hata hayo yasiyo safi nayo ni shida kuyapata.

Hakuna anayekatazwa kusifia anachohisi kinastahili kusifiwa lakini ingekuwa vizuri kama utolewaji wa sifa hizo unazingatia uhalisia wa sifa zinazotolewa.