Friday, 21 March 2014

Waalimu wala maisha ya kifalme Kigoma, waahidiwa mambo rukuki ambayo haijawahi kutokea. Ebu twende hapa, vitendo anakusubiri upate mengi.

Katika utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Halmashauri ya Wilaya Kigoma, imeamua kuwapokea walimu wapya 430, kwa mbinu ya pekee ili wabaki katika vituo vyao vya kazi.

Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya Kigoma, Miriam Mbaga, alitangaza mbinu hizo jana wakati alipozungumza kwenye kikao cha maandalizi
ya mapokezi hayo.

Alisema pamoja na maandalizi mengine, halmashauri hiyo imetenga Sh milioni 25 kwa ajili ya kuwapa walimu hao fedha za kujikimu wakati wakishughulikia maandalizi ya kwenda kwenye vituo vyao vya kazi.

Fedha hizo ni nje ya kiwango cha fedha kilichotengwa na Serikali kwa ajili ya kujikimu, ambacho kila mwalimu atakayeripoti atapewa kimsaidie kujikimu kwa siku saba.

Sambamba na posho hiyo, Mkurugenzi huyo alisema kuwa pia katika kuhakikisha wanawapokea walimu wao kifalme, halmashauri itampatia kila mwalimu godoro
moja na taa ya kuchaji, ambavyo vinatolewa kama motisha kwa walimu hao wapya.

Mbaga alisema kuwa wakati.motisha hiyo ikitolewa, pia timu ya watumishi wa halmashauri imejipanga kuwapokea walimu
watakaoripoti katika vituo vya mabasi na kituo kikuu cha reli mjini Kigoma.

Wakati wa mapokezi hayo, watumishi hao watakwenda katika vituo husika wakiwa na mabango yanayoashiria mapokezi ya walimu
na baada ya kuwapokea,watawapeleka katika nyumba za kulala wageni watakapoishi wakisubiri utaratibu wa kiutumishi wa kuwapatia makazi.

Mkurugenzi huyo wa halmashauri
amebainisha kwamba wakati katika ngazi ya halmashauri maandalizi yakiendelea hivyo,
katika ngazi za vijiji, viongozi wa vijiji wamekutana na kuanza maandalizi ya kuwatafutia walimu wapya nyumba za kuishi zenye hadhi ya kuishi walimu hao kwa ngazi ya kijiji.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigalye, kilichopo Kaskazini ya Mwambao wa Ziwa Tanganyika, Hussein  Mussa Kasala, alisema tayari
Halmashauri ya Kijiji hicho imekutana na kutafuta nyumba nne.

Nyumba hizo kwa mujibu wa Kasala, zinakidhi mahitaji ya familia nane za walimu hao; zimejengwa kwa matofali na zipo katika mazingira mazuri ya kuishi
walimu.

Mwenyekiti huyo wa Kijiji alisema kuwa wanakijiji wamejipanga kuwapokea walimu hao kwa kuwapatia magunia ya mahindi na
maharage, kwa ajili ya kuanzia maisha huku wavuvi wakiahidi kuwapatia samaki na dagaa kila watakapokuwa wakirudi kutoka
ziwani.

Akielezea hali hiyo, Mbaga alisema kuwa utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, unaanzia kwa mtu mmoja mmoja kama ambavyo halmashauri za vijiji
zimeamua kuchukua hatua kutekeleza jambo hilo kulingana na rasilimali zinazowazunguka.

Naye Meneja wa benki ya CRDB, tawi la Kigoma, Philemon Pindapinda, ambaye alikuwa mmoja wa viongozi wa sekta binafsi
na sekta ya umma walioalikwa kuhudhuria maandalizi ya mapokezi hayo, alisema hatua
iliyofikiwa itawatia moyo walimu kuona namna ambavyo utumishi wao unakuwa na maana kwa jamii.

Pindapinda alisema nia ni kuona walimu wanaopangiwa mkoani humo hasa katika maeneo yanayoonekana kuwa na miundo
mbinu duni ya usafiri, wanaripoti na kukubali kuishi katika mazingira hayo na kufanya kazi yao kwa moyo.

Mhasibu Mkuu wa Benki ya Posta (TPB) tawi la Kigoma, Ahmed Soso, alisema maandalizi yanayofanywa na Halmashauri ya Wilaya Kigoma, yanapaswa kuwa mfano wa kuigwa
na halmashauri nyingine za mkoa huo, ili kuwaonesha moyo wa upendo watumishi hao wa sekta ya elimu ili waripoti na kukaa kwenye vituo walivyopangiwa badala ya
kukimbia.