Monday, 31 March 2014

Njia 60 za daladala kusitishwa Dar es salaam. Twende hapa na vitendo upate mengi zaidi.

Njia 64 za magari ya daladala jijini Dar es Salaam zitakoma kutumika kutokana na kuanza kwa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART).

Kwa kuanzia matayarisho ya kupisha mradi huo, Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo
Haraka Dar es Salaam (DART) umetaka wamiliki wote wa mabasi ya daladala yanayopita katika Barabara ya Morogoro au
kukatiza katika njia hiyo, kufika katika ofisi zake kujiandikisha.

Mhandisi wa Wakala , John Shauri
aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kuwa wamiliki hao wanatakiwa kufika katika ofisi za Dart zilizoko jengo la Ubungo Plaza barabara ya
Morogoro kuanzia leo hadi Aprili 21 mwaka huu kwa ajili ya kujiandikisha kama moja ya
matayarisho ya kupisha mradi huo.

Dart iko kwenye mchakato wa kuwezesha upatikanaji wa watoa huduma kwenye mfumo mpya wa mabasi yaendayo haraka awamu ya kwanza ambayo inajumuisha
barabara ya Morogoro, Kawawa na Mtaa wa Msimbazi kwa njia kuu na nyingine za kiungo.

Alisema kulingana na mpango wa
uendeshaji wa mfumo wa Dart, barabara zinazohusika zitapaswa kutumiwa na mabasi ya mfumo huo pekee.

“Wakala umemwajiri mtaalamu mshauri kuwezesha wamiliki wa daladala kuelewa vizuri mfumo na kujipanga kuwa washiriki kwenye mfumo huu mpya,” alisema.

Shauri alitaja baadhi ya njia zitakazoguswa na ni pamoja na Mbagala Rangi 3 kwenda Masaki, Vingunguti kwenda Makumbusho,
Kunduchi Kwenda Mwenge, na Msata kwenda Ubungo. Njia nyingine ni Kariakoo kwenda Makumbusho, Buguruni kwenda
Kawe, Kivukoni kwenda Mburahati, Mbagala Kuu kwenda Mwenge, na Mkata kwenda Ubungo.

Njia nyingine ni Mburahati kwenda
Muhimbili, Segerea kwenda Mwenge, Vingunguti kwenda Kawe, Vingunguti kwenda Mbezi, Kunduchi kwenda Posta, na Kunduchi kwenda Makumbusho.

Pia alitaja Temeke kwenda Masaki, Kivukoni kwenda Mabibo, Muhimbili kwenda Mabibo, Posta kwenda Ubungo, Posta kwenda
Mabibo, Kawe kwenda Kimara, Kivukoni kwenda Mbezi, Mwenge kwenda Mbezi, Posta kwenda Mbezi, Mbezi kwenda Tegeta na
Bunju kwenda Makumbusho.

Alisema wamiliki hao wa daladala
wanahitajika kwenda na nakala ya leseni ya Sumatra , nakala ya usajili wa gari, na nakala za rangi za leseni za madereva wao.
Uandikishaji utakuwa unafanyika kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa asubuhi saa 3 mpaka saa 11 jioni.
Kwa siku za Jumamosi na Jumapili
uandikishaji utakuwa unafanyika kuanzia saa 3 asubuhi mpaka saa 8:30 mchana.

Mshauri Elekezi wa Wakala , Felix Mlaki alisisitiza wamiliki hao kufika ofisi za Dart kujisajili na kufafanua kuwa daladala hazitasajiliwa tena na Sumatra katika eneo la mradi huo.

“Tunawahitaji wajisajili na pia watoe mawazo yao juu ya kuanza kwa awamu ya kwanza ya mradi huu wa mabasi yaendayo haraka,”alisema Mlaki.

Alisema mradi huo ni wa kisasa na una manufaa makubwa kwa wananchi. Alisema mfumo huo unatoa utaratibu mzuri wa ukataji tiketi na utoaji taarifa sahihi kwa
abiria.