Monday, 3 March 2014

Joel Bendera: Wafichueni waandishi makanjanja.

Wahitimu wa Uandishi wa Habari wa Chuo cha Uandishi wa Habari Morogoro (MSJ) wametakiwa kuwafichua waandishi wa habari wasio na sifa, wanaojiingiza kwenye
tasnia ya habari.

Imeelezwa kuwa waandishi hao wasio na sifa, wanaifanya taaluma hiyo ionekane kuwa ni ya uchochezi mbele ya jamii na iliyokosa mwelekeo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, katika hotuba yake iliyosomwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Eliya Ntandu.

Alisema hayo kwenye mahafali ya 17 ya Chuo cha Uandishi wa Habari Morogoro (MSJ) yaliyofanyika juzi, mjini hapa. Mkuu wa Mkoa alipongeza uongozi wa chuo hicho.

Pia alipongeza wahitimu wote kwa kazi ngumu walioifanya, uvumilivu, juhudi, maarifa, nidhamu na kujituma na kuwawezesha kuhitimu masomo yao katika Mahafali hayo.

"Kama mnavyofahamu nchi yetu ina waandishi wengi wa habari wasio na sifa, wengi wao ni wale waliojiingiza katika tasnia ya habari na kuifanya taaluma hii ionekane kuwa ni ya uchochezi na iliyokosa muelekeo" alisema Mkuu wa Mkoa.

Alisema mahafali hayo yameudhihirishia umma kuwa sasa taifa limepata watu sahihi watakaoungana na waandishi wengine, ambao wanafanya kazi kwa kutambua kuwa tasnia ya habari ni muhimu na ina mchango
mkubwa katika kuleta maendeleo ya taifa.

Mkuu wa chuo hicho, Augustine Nongwe, alisema jumla ya wahitimu 121 walitunukiwa
vyeti, wakiwemo wa Uandishi wa Habari ngazi ya Stashahada, na Cheti.

Wengine ni katika kozi ya ualimu wa elimu ya awali. Alisema chuo hicho kimetimiza miaka 19 tangu kianzishwe mwaka 1995 kwa
kutoa kozi mbalimbali, ikwemo ya Uandishi wa Habari na Ualimu wa elimu ya awali, uhusiano na masoko.

Chanzo: Habari Leo.