Serengeti “Ni zaidi ya miezi sita tangu nifanyiwe ukatili na mume wangu na mama mkwe.Nahangaika kuuguza mguu niliokatwa kwa panga kunyunyiziwa maji ya betri, sijui kama utapona. Kichanga nacho kinasumbua, jamani nimekosa nini mimi kwa Mungu.”
Ni maneno yenye kutia simanzi na ambayo yanaamsha kilio. Maneno ya ya Anna Sabai (20) mkazi wa Kitongoji cha Manyata Kijiji cha
Nyamakendo Kata ya Mbalibali, wilayani Serengeti, ambaye anapaza sauti kutaka kujua
walipo wanaharakati ambao kwa hali aliyonayo , angeweza kupata msaada kutoka kwao.
Ukatili aliofanyiwa Anna, mama wa watoto wawili katika ndoa yake na Hamisi Sabai (20) yenye migogoro na ambayo inazidi kuuweka
Mkoa wa Mara kwenye taswira mbaya kutokana na uwingi wa matukio ya ukatili dhidi ya wanawake.
Agosti Mosi, 2013 ikiwa ni siku ambayo wakazi wa wilaya hiyo humiminika mnadani, Anna
akiwa na uja uzito wa miezi tisa na akihesabu siku tu kwa ajili ya kujifungua, aliamriwa na
mume wake kwenda kuchunga ng’ombe, bila kujali hali yake.
“Kwa kweli nilikuwa na hali mbaya sana,” anakumbuka Anna wakati anaongea na Mwananchi kuhusu ukatili dhidi yake.
“Nikiwa malishoni nilikaa chini ya kivuli huku ng’ombe wakiendelea kula majani. Hali ilivyozidi kuwa
mbaya nilisinzia. Alipokuja mume wangu akanikuta nimelala na hapo hapo akaanza kunishambulia kwa kipigo, akidai kuwa nilikuwa na mwanamume kutokana na
mapenzi kunoga ndio maana nilisinzia na kuacha ng’ombe wanazagaa.”
Anasema pamoja na kujieleza na kwa kuzingatia hali yake, walipofika nyumbani mama mkwe wake Bhoke Sabai alizidi kumtia
hasira kijana wake akidai kuwa nilikuwa na mwanaume, natakiwa kupewa kipigo ili iwe fundisho.
“Pamoja na kuwa wakati ananipiga sikuwa najitetea, bado akaona aache fimbo na akachukua panga na kunikata mguu wa kushoto,” anasema Anna huku akitokwa na
machozi.
“Niliumia sana... nikatamani kufa, maana hali ilikuwa mbaya. Sikuwa na msaada. Baadaye akanifungia ndani ili watu wasijue; wala hakuna kwenda kutibiwa.”
Amwagiwa tindikali ili kuzuia damu isitoke huku akiwa amebeba mtoto wake na kutembea kwa shida,Anna anasema ili watu wasijue unyama aliotendewa, walileta maji ya betri na kumwagia kwenye kidonda.
“Maumivu yalikuwa zaidi ya uchungu wa kujifungua. Nilifikia hatua kama ningepata kitu
cha kujimaliza, ningejiua. Nilikuwa
nasumbuliwa na mimba na huku naumizwa hivi,” analalamika.
“Jamani wanaharakati wanaotetea wanawake wako wapi maana
nitakatwa mguu hivi hivi.”
Anasema matokeo yake mguu ukaoza kwa kuwa alikaa ndani muda mrefu na kwamba ndugu zake hawakuambiwa na mama mkwe wake alikuwa akiendelea kumkejeli kila
wakati.