Baraza la Sanaa la Taifa (Basata),
limeitaka Kamati ya Miss Tanzania
kutohusisha burudani zinazokiuka
maadili ya Mtanzania wakati wa
mashindano yao mwaka huu.
Akizungumza wakati wa kikao cha
tathmini ya mashindano ya Miss
Tanzania 2013 kilichofanyika kwenye ukumbi wa baraza hilo, Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Idaya ya Ukuzaji Sanaa Basata, Vivian Shalua,
Alisema kuwa, maadili ni muhimu kuzingatiwa katika mashindano hayo ili kuepukana na dhana potofu kuwa, yanahusiana na
uhuni.
“Maadili yazingatiwe katika mashindano ya mwaka huu, kuanzia kwa washiriki hadi burudani zitakazohusishwa, kama
‘vigodoro’, ‘kanga moja mbendembende’ na nasikia siku hizi kuna ‘tisheti ndembendembe’,” alisema mkurugenzi huyo.
Alisema kuwa, Basata ipo tayari
kuyapigania mashindano ya Miss
Tanzania kuhakikisha yanakuwa katika ubora wa hali ya juu, kwa kushirikiana na Kampuni ya Lino International Agency ambao ndio waandaaji.
Mkurugenzi huyo pia aliitaka Lino
kuwaelimisha mawakala wanaoandaa mashindano hayo juu ya umuhimu wa kuwa na vibali kutoka Basata, ikiwa ni
pamoja na kutowavumilia watovu wa nidhamu bila kujali ukongwe wao katika tasnia hiyo.