Muuguzi Lucia Ilomo (44) amehukumiwa kifungo cha miaka 28 jela katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam baada ya kupatikana na hatia ya kughushi vyeti vya Uuguzi na Ukunga.
Hakimu Mkazi Augustina Mmbando alitoa hukumu hiyo jana baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi watatu wa upande
wa Jamhuri pamoja na utetezi wa
mshitakiwa.
Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Mmbando alisema upande wa Jamhuri umethibitisha mashitaka manne dhidi ya mshitakiwa na
katika kila shitaka atatumikia kifungo cha miaka saba jela.
Hata hivyo, alisema Lucia ambaye pia anajulikana kwa jina la Veronica Kuyena, atatumikiwa adhabu hizo kwa wakati mmoja
hivyo ni sawa na kifungo cha miaka saba jela.
Lucia alikuwa anakabiliwa na mashitaka sita ya kughushi, kuwasilisha vyeti vya kughushi
na kujitambulisha kuwa yeye ni mtu mwingine hata hivyo alipatikana na hati ya mashitaka manne.
Ilidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Februari 2007 na Mei mwaka jana Dar es Salaam, alighushi cheti cha uuguzi chenye
namba 18558 na cheti cha ukunga namba 13568 akionesha kuwa vimetolewa kwake kama Lucia Kazohela jambo ambalo si kweli.
Katika mashitaka mengine ilidaiwa kuwa katika tarehe hizo, mshitakiwa alijitambulisha kuwa yeye Lucia Kazohela kwa kuwasilisha vyeti vya uuguzi na Ukunga akidai kuwa ni vya kwake jambo ambalo si kweli.
Aidha ilidaiwa kuwa, aliwasilisha vyeti hivyo kwa Ofisa Rasilimali watu wa Manispaa ya Kinondoni.
Katika utetezi wake, Lucia alidai kuwa alisoma katika Chuo cha Uuguzi cha Mvumi mwaka 1980, jana aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ana mtoto anayemtegemea.