Thursday, 20 November 2014

Sitta: Mbunge Shy-Rose hakupigana Kenya

Serikali imesema Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Shy-Rose Bhanji hajapigana nchini Kenya, na wanasubiri Tume ya EALA ili kujua ukweli wa tuhuma zinazoelekezwa kwake.

Kwa muda sasa, Shy-Rose amekuwa katika mzozo na wabunge wenzake wa EALA, kwanza akituhumiwa kuwatukana wakiwa safarini Ubelgiji na juzi akituhumiwa kupigana na mwenzake kutoka Tanzania, Dk Nderakindo Kessy.

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta awali alilieleza Bunge jana mjini hapa kuwa kiini cha mzozo wote ni mgogoro dhidi ya Spika wa EALA, Margaret Zziwa wa Uganda.

Sitta alisema yapo makundi mawili sasa ndani ya Bunge hilo, moja likitaka kumng’oa Spika huyo na lingine likimkingia kifua kwamba hapaswi kuondolewa.

“Katika hili (la kumng’oa Spika), Tanzania ni kikwazo, kwa sababu ili Spika aondolewe ni lazima akidi itimie, na akidi hiyo ni kupata kuungwa mkono kwa idadi fulani ya wajumbe wa kila nchi. “Sasa Tanzania wamefuta hoja ya kutaka Spika huyo aondolewe na hii ndiyo imesababisha chuki yote,” alieleza Sitta kabla ya kujibu hoja kuhusu Shy-Rose.

Sitta alisema Shy-Rose hakupigana au kumpiga mbunge mwenzake kama ilivyoandikwa katika magazeti jana.

Alisema kilichotokea kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Naibu Waziri wa wizara hiyo, Abdallah Sadalla, Shy-Rose alimsukuma kwa bahati mbaya Dk Kessy wakati akiwahi usafiri, ndipo mwenzake akahamaki.

“Hili la juzi, kwa mujibu wa Naibu Waziri, siyo sawa na kilichoelezwa. Shy-Rose inafahamika kuwa ni mfuasi mkubwa wa yule Spika (Zziwa). “Yeye alikuwa akiwahi usafiri, hivyo akawakuta wenzake na alipopita kwa haraka, kwa bahati mbaya akamsukuma Kessy, ambaye alihamaki, hivyo kwa msaada wa wabunge wa Uganda wakalichukua na kutoa taarifa kwamba alifanyiwa assault (shambulio la kudhuru mwili).

“Lakini baadaye walilimaliza ndani ya Bunge baada ya wawili hawa kusikilizana na Polisi wakaondoa shauri hilo,” alifafanua Sitta na kuongeza: “Kwa haya mambo mengine ya ovyo anayodaiwa kufanya mheshimiwa yule, hivi sasa kumeundwa Tume ya Bunge la Afrika Mashariki, hivyo sisi hapa hatuwezi kufanya chochote.

Via HabariLeo