Tuesday, 18 March 2014

Wananchi Zanzibar wakataa serikali 3. Mfuate vitendo hapa upate mengi juu ya hili.

Asilimia 60 ya wananchi wa visiwani Zanzibar waliotoa maoni yao kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wametaka muundo wa Muungano wa serikali ya mkataba na hakuna hata mwananchi mmoja aliyetaka muundo wa serikali tatu.

Kwa upande wa Tanzania Bara asilimia 61 walitaka muundo wa serikali tatu, na hakuna aliyependekeza muundo wa serikali
ya mkataba.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Jaji mstaafu Joseph Warioba, wakati anawasilisha maoni ya wananchi na taasisi
mbalimbali yaliyokusanywa na Tume yake kwa Bunge Maalum la Katiba, alisema karibu wananchi wote waliotoa maoni kwa upande
wa Zanzibar walijikita kuhusu Muungano.

“Kati ya wananchi karibu 38,000 waliotoa maoni kuhusu Muungano, wananchi 19,000 Zanzibar walitoa maoni kuhusu muundo wa
Muungano. Asilimia 34 walipendekeza serikali mbili asilimia 60 muungano wa
mkataba na wananchi 25 sawa na asilimia 0.01 walipendekeza serikali moja,” alifafanua Jaji Warioba.

Jaji Warioba alisema taasisi nyingi kama vyama vya siasa, asasi za kiraia na jumuiya za kidini zilipendekeza muundo wa serikali
tatu.

Alisema kwa upande wa Tanzania Bara, wananchi wengi waliotoa maoni kuhusu Muungano walijikita kwenye Muundo wake kama njia ya kuondoa kero ambapo zaidi ya
wananchi 39,000, walitoa maoni kuhusu Muungano na kati ya hao karibu 27,000 walizungumzia muundo.

Alisema asilimia 13 walipendelea serikali moja kwa Tanzania Bara huku asilimia 24 wakitaka serikali mbili na asilimia 61 serikali tatu.

“Suala la muundo wa serikali tatu
limechukua nafasi kubwa sana katika mjadala tangu Tume ilipozindua Rasimu ya Kwanza ya Katiba.Mjadala wa muundo wa
Muungano umekuwa mkubwa kwa kiasi cha kufunika mapendekezo mengine yaliyomo katika Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano,” alisema.

Jaji Warioba alisema Tume yake iliamini Sheria ya Mabadiliko ya Katiba katika kifungu cha 9(2) iliyotoa mwongozo wa kuendelea kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano, uwepo wa Serikali, Bunge na
Mahakama na Serikali ya Mapinduzi ulikuwa
mwongozo wa Tume yake na si kwa
wananchi.

“Tume iliamini sheria haikukusudia
kuwazuia wananchi kutoa mawazo yao kwa uhuru bila ya kizuizi wala mipaka hivyo ilipokea mawazo ya kila aina,” alisema.

Alisema Tume ilifuata njia ya wananchi kuwa huru katika kutoa maoni yao kwa kuwaruhusu kusema chochote kuhusu
maeneo yao, ikiwa ni pamoja na suala la Muungano na kutowapa muongozo kama kujibu maswali kwa njia ya madodoso.

Wakati huohuo Warioba ameeleza kwamba taasisi za Serikali zilizowasilisha mapendekezo yao kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ikiwemo Ofisi ya Waziri
Mkuu Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na Ofisi ya Makamu wa Rais, zimependekeza mfumo wa serikali tatu.

Alilitaja Baraza la Wawakilishi na kueleza kuwa lilipendekeza kuwepo mamlaka huru ya Zanzibar, Tanganyika na mamlaka ya
Muungano na kutaka iwekwe wazi maeneo, uwezo, nguvu, utendaji na mipaka ya mamlaka.

Alitaja Baraza la Ofisi ya Waziri Mkuu, ambalo lilipendekeza kuhusu uongozi wa Taifa kwa kutaka kuwe na Rais wa Jamhuri
ya Muungano, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Waziri Mkuu wa Serikali ya Tanganyika na Waziri Mkuu wa Serikali ya
Zanzibar.

Katika mapendekezo yao Ofisi wa Waziri Mkuu, Warioba alisema walieleza ni kwa sababu hakuna umuhimu wa kuwa na marais watatu katika nchi moja na wala
neno rais halimuongezei hadhi kiongozi yeyote.

Mapendekezo yao pia yalitaka mawaziri wakuu hao wapewe nafasi kuwa watendaji zaidi na hivyo kusimamia serikali za
washirika.

“Ofisi ya Makamu wa Rais,ilipendekeza kuwe na Rais mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wakuu wa serikali za washirika wa Muungano wapewe
vyeo vingine, vinavyoendana na hadhi na mamlaka zao. Pia katika kutaja hizo serikali tatu inabidi zitenganishwe ili serikali ya
Muungano ionekane ndiyo ya juu,” alisema Warioba.

Mbali na hao, Bunge la Jamhuri ya
Muungano lilipendekeza kuwepo kwa Tume ya Utumishi wa Bunge, ambayo inajumuisha wajumbe, Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano(Mwenyekiti), Spika wa Bunge la Tanzania Bara na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba (kushoto) akibadilishana mawazo na Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba (kutoka kushoto kwake) Freeman Mbowe, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mathias Chikawe, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samia Suluhu Hassan baada ya kuwasilisha Rasimu ya Pili ya Katiba bungeni mjini Dodoma jana. Chanzo. HabariLeo