Watu watano, wakiwemo wanawake wawili wanaodaiwa kukodi wauaji, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Hakimu Mkazi ya Nkasi, mkoani Rukwa. Wote wanatuhumiwa kula njama ya kuua kwa imani za kishirikina kwa malipo ya Sh milioni 3.
Walifikishwa mahakamani juzi kwa mara ya kwanza mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo Ramadhani Mgalamalila. Watu hao ni Specioza Mwanandenje (55) mkazi wa kijiji cha Swaila wilayani Nkasi na Editha Benedicto (20), mkazi wa kijiji cha Kisura wilayani Nkasi.
Wengine ni John Paulo (28) mkazi wa Kalumbaleza wilayani Sumbawanga mkoani
Rukwa, Linga Luhende (26) mkazi wa Kisiwani, Manispaa ya Sumbawanga na Ngasa Mahona (24) , mkazi wa kijiji cha Majimoto wilayani Melele mkoa wa Katavi .
Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi wa Polisi, Hamimu Gwelo alidai kuwa washtakiwa hao watano walikamatwa Februari 28, mwaka
huu kijijini Kisura nyumbani kwa mshtakiwa wa pili , Editha kwa kula njama ya kumuua Selisi Kipini (75) aliyekuwa akituhumiwa na
washtakiwa hao wawili kuwa alikuwa akiuua watoto wao kichawi.
Gwelo alidai kuwa washitakiwa Spesioza na Editha waliwakodisha vijana wa kiume John, Linga na Ngasa kumuua Selisi Mpini kwa
gharama ya Sh milioni 3, lakini kwa mkopo, kwa kuwa hawakuwa na fedha taslimu kwa wakati huo, hivyo wangelipwa baada ya
kufanya mauaji.
Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao, waliombwa walipwe kianzio cha Sh milioni 2.5 ili waweze kufanya mauaji hayo, lakini wanawake hao walidai kuwa kiasi hicho cha
fedha hawakuwa nacho wakati huo, hivyo waliwabembeleza wakubali kufanya mauaji hayo kwa mkopo.
Mwendesha Mashtaka alidai vijana hao wa kiume, baadaye walibadilikia wanawake hao
na kuwaambia kuwa watawaua siku hiyo Februari 28, mwaka huu nyakati za usiku, kwa kuwa wameshindwa kuwalipa fedha zao
na kuwapotezea muda. Vijana hao walidai kwamba hawakuwa tayari kuua kwa mkopo.
Alidai kuwa mabishano hayo, yalifanyika nyumbani kwa Editha kijijini Kisura, ambapo msichana (jina lake limehifadhiwa)
alikuwemo ndani ya nyumba hiyo na alisikia yote yaliyozungumzwa.
Alidai msichana huyo alitoa taarifa kwa uongozi wa Serikali ya Kijiji hicho.
"Uongozi wa Serikali ya kijiji hicho uliitaarifu Polisi usiku wa Februari 28, kuwa kuna uwezekano yakatokea mauaji kijijini Kisura
hivyo saa tatu usiku wa usiku huo polisi walifika eneo la tukio na washtakiwa wote watano wakiwa ndani ya nyumba hiyo ya
mshtakiwa wa pili walikamatwa na
kufikishwa katika Kituo cha Polisi mjini Namanyere," alidai Gwelo mahakamani hapo.
Licha ya dhamana kuwa wazi kwa
washtakiwa wote watano, Mwendesha Mashtaka alipinga wasipewe dhamana.
Alidai kuwa bado kuna washitakiwa
wengine, ambao bado hawajakamatwa na wametajwa na washtakiwa waliokamatwa, kuwa ni wana mtandao wanaofanya mauaji
kwa kukodishwa.
Hamimu Mgalamalila alikubaliana na ombi hilo la MwendeshabMashtaka na kuamuru washtakiwa hao warudishwe rumande hadi Machi 20 , mwaka huu shauri lao litakapotajwa tena.