RAIS Jakaya Kikwete amesema changamoto mojawapo iliyopo nchini katika kupambana na ujangili, ni ukubwa wa hifadhi na
kutokuwa na rasilimali watu wa kutosha.
Rais Kikwete alisema hayo jana wakati akipokea msaada wa magari mapya 11 aina ya Land Rover kutoka kwa Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) la nchini Ujerumani.
Alisema kati ya eneo lote la nchi lenye ukubwa wa kilometa za mraba takribani 945,000, eneo la kilometa za mraba 159,817.02 ni maeneo ya hifadhi ambayo yana wanyama kama tembo ambao
wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ujangili.
Alisema licha ya kuwa na eneo kubwa la hifadhi, lakini rasilimali watu ni wachache ambapo kwa wastani, mtu mmoja anasimamia kilometa za mraba 168 wakati
kwa viwango vya kimataifa mtu mmoja kusimamia kilometa za mraba 25 pekee.
Rais alisema rasilimali watu waliopo ni asilimia 24 pekee ya wanaohitajika ambao ni 4,000, hivyo juhudi zimeanza kwa kuajiri
watumishi hao na lengo linatarajiwa kufikiwa mwaka 2016.
“Baada ya kuajiri rasilimaliwatu wa kutosha, changamoto itakayobakia ni vifaa na mafunzo maalum katika kukabiliana na vitendo hivi vya ujangili …ninazidi kuwasihi
marafiki zetu hawa kuendelea kutusaidia ili kufikia malengo yetu ya kushinda vita hivi na siyo kushindwa,” alisema Rais Kikwete.
Alisema sekta ya utalii inachangia katika Pato la Taifa (GDP) kwa asilimia 17 huku ikitoa ajira kwa wananchi zaidi ya 300,000 na kusisitiza operesheni mbalimbali za
kupambana na ujangili zitaendelea.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema Operesheni Tokomeza inatarajiwa kuanza wakati wowote na siyo siri mara itakapoanza itatangazwa.
Aliwataka wafugaji katika maeneo hifadhi kutoa mifugo yao kwani hawaruhusiwi kisheria na watakaokutwa ndani ya hifadhi
katika operesheni hiyo, wawe mifugo au watu hawataachwa.
Nyalandu alisema msaada huo wa magari ni sehemu ya mchango wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotolewa na taasisi za kijerumaini ambazo jumla yake ni Euro milioni 20 kusaidia kukabiliana na ujangili nchini.
Mkurugenzi FZS Afrika, Robert Muir alisema magari matano kwa ajili ya hifadhi ya Serengeti, matano kwa asili ya Kanda tano
katika hifadhi za Selous na moja kwa ajili ya hifadhi ya Maswa.
Alisema msaada inalenga kuongeza nguvu katika kupambana na majangili hao baada ya kushiriki katika sensa iliyofanyika hivi karibuni na kubaini kupungua kwa kasi kwa
idadi ya tembo nchini.
Siku za karibuni serikali ilitoa magari zaidi ya 20 aina ya Toyota Land Cruiser kwa ajili ya kukabiliana na ujangili katika baadhi ya hifadhi za taifa nchini.
Hatua hiyo ni mpango wa serikali kutekeleza kwa vitendo mapambano dhidi ya ujangili
iliambatana na kukombolewa kwa bunduku 500 aina ya AK 47 zilizokuwa chini ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tangu
Novemba 2012.
Bunduki hizo zilikuwa zinashikiliwa na TRA kutokana na kutolipiwa kodi na kuwa tayari wizara imetoa sh. milioni 212 kwa ajili ya
kulipa kodi na ushuru.Bunduki hizo
zimegharimu Sh milioni 427.
Mbali na magari hayo yaliyotolewa na washirika, Mfuko wa Wanyamapori umenunua magari 14 aina ya Toyota yenye
thamani ya Sh bilioni 1.6 ambayo
yamegawanywa katika maeneo mbalimbali.