Bunge jana liliahirishwa kwa mara tatu mfululizo, kutokana na kutoafikiana juu ya mapendekezo yaliyotolewa dhidi ya wahusika wa sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa katika Benki Kuu Tanzania (BoT).
Katika sakata hilo ambalo lilianza kujadiliwa Jumatano wiki hii, wabunge walikuja juu wakitaka fedha zilizochukuliwa katika akaunti hiyo, zirejeshwe na wahusika wachukuliwe hatua ya kuvuliwa nyadhifa zao.
Pamoja na kurejeshwa, pia wabunge hao wamekuwa wakilalamikia utoaji wa fedha hizo kutoka katika akaunti hiyo, bila kufuata taratibu ikiwemo kutolipwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Katika majadiliano hayo, wabunge walisema fedha hizo ni za umma huku Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, wakieleza Bunge kuwa si fedha za umma.
Hali hiyo ilileta mvutano mkubwa ndani ya Bunge, kiasi cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikai (PAC), kuandaa mapendekezo katika kutatua mvutano huo.
Awali juzi usiku, Bunge kwa mara ya kwanza liliendelea na kikao chake hadi saa tano kasoro usiku, kujadili mapendekezo ya maazimio ya Bunge, yaliyotolewa na PAC.
Sababu kubwa ya Bunge kufikia muda huo, ilikuwa mvutano katika baadhi ya mapendekezo yake, ikiwemo kuvunjwa kwa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kutenguliwa kwa uteuzi wa Profesa Muhongo, Jaji Werema na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi.
Baadhi ya mapendekezo ya PAC yalikubaliwa na wabunge, lakini pendekezo lililosababisha Bunge kuahirishwa lilihusu kutenguliwa kwa nafasi ya Profesa Muhongo.
Wakati wakijadili kuhusu pendekezo hilo, baadhi ya wajumbe walishauri uteuzi wa waziri huyo utenguliwe, huku wengine wakisema mamlaka yenye kumteua ndio yenye madaraka ya kutengua au la.
Hata hivyo, Spika Anne Makinda aliomba ushauri jinsi ya kuweka suala hilo, ili lisiendelee kuingilia mihimili mingine. Kutokana na hilo, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM) alitoa mapendekezo kuwa Bunge lipendekeze kwa mamlaka iliyomteua, kuchukua hatua zaidi itakapobainika kuna makosa yamefanyika.
Hali hiyo ilisababisha mvutano mkubwa na mwishowe Mwenyekiti wa PAC, Kabwe Zitto, aliunga mkono pendekezo hilo, huku wabunge wengi wa Kambi ya Upinzani, wakikataa na kuanza kupiga kelele kuwa ‘wezi wote waondoke’.
Makelele hayo toka kwa wabunge wa Kambi ya Upinzani, yalimfanya Spika Anne Makinda, kuahirisha Bunge hadi jana saa tatu asubuhi.
Hata hivyo, jana asubuhi Bunge hilo lilishindwa kuendelea baada ya Spika kutaka pande mbili za wabunge kukutana katika vikao vya vyama kujadili suala hilo.
Spika aliahirisha Bunge hilo hadi saa tano asubuhi, lakini hata hivyo hakukuwa na muafaka hivyo Spika akazitaka pande mbili za wabunge, kutoa wajumbe wao wachache, ili waende kujadiliana kuhusu mapendekezo hayo na kuja na msimamo mmoja kama Bunge.
‘’Waheshimiwa wabunge ili twende vizuri, tumeona ni vyema pande hizi mbili zichague viongozi wachache wakae pamoja na kujadili mapendekezo haya, ili jioni tuje na jambo la pamoja kama Bunge moja,’’ alisema Makinda.
Spika Makinda aliahirisha Bunge hadi saa 10 jioni jana, lakini akalazimika kukiahirisha tena hadi saa moja usiku jana na baadaye muafaka kupatikana na Bunge kuahirishwa.