Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imesema iko tayari kusaidia vijana watakaojiunga katika vikundi vya ujasiriamali kwa kuwapa mikopo nafuu kutoka kwenye mfuko wa maendeleo ya vijana ulioanzishwa na wizara hiyo.
Kutokana na changamoto ya ajira nchini, Wizara imesema iko tayari kutoa mikopo kati ya Sh milioni 50 hadi 100 kwa vijana watakaojiunga katika vikundi vya ujasiriamali.
Akizungumza katika mahafali ya sita ya Taasisi ya Maendeleo na Usimamizi wa Maji (WDMI) kwa niaba ya Waziri, Dk Fenella Mukangara, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Elisante ole Gabriel alisema, suala la ajira limekuwa ni tatizo hivyo kuna wajibu wa vijana kujitambua na kujiajiri wenyewe.
Alisema ukosefu wa ajira kwa vijana ni asilimia 11.7 ambapo alifafanua kuwa kwa vijana walioko mijini ni asilimia 16.7 na vijijini 7.5, kwa mkoa wa Dar es Salaam peke yake ukosefu wa ajira ni asilimia 31.5.
“Kujiriwa kwa kijana sio kupata maendeleo moja kwa moja bali ajira inaweza ikawa sehemu ya maendeleo ya vijana, tatizo vijana wengi wanakabiliwa na fikra hafifu wengi wao wanadhani maendeleo yataletwa na serikali kwenye sahani na wao hawahusiki,” alisema Profesa Gabriel.
Katika mahafali hayo ambayo walihitimu vijana 217 ngazi ya Stashahada , aliwataka kutumia vizuri elimu yao kwani kuna uhusiano mkubwa kati ya uchumi wa nchi pamoja na maji. Alisema uwajibikaji ndio utaweza kuwapa heshima na hawataweza kuheshimika kwa kuwa na Stashahada.