Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema suala la kumtaka ajiuzulu wadhifa wake si jipya, lakini akasema ni vyema kusubiri mjadala wa Bunge wa sakata la Tegeta Escrow ufike mwisho, ndipo hatua stahiki zitajulikana.
Waziri Pinda alisema hayo jana wakati akijibu maswali katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu alipoulizwa kama haoni ni wakati wake kuwajibika kwa sakata hilo.
Maswali hayo yalielekezwa kwake saa chache baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwasilisha maoni yake kuhusu matokeo ya ukaguzi maalumu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Katika maswali yake kwa Pinda jana, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alimtaka Waziri Mkuu kujiweka pembeni na kupisha wengine kutokana na kile alichoeleza kuwa ni Serikali yake kukumbwa na kadhia nyingi kuanzia Operesheni Tokomeza, mauaji ya watu Kiteto mkoani Manyara na sasa sakata la Tegeta Escrow.
Hata hivyo, Waziri Mkuu Pinda alisema: “Kujiuzulu ni suala linaloweza kutokea kama Mungu akipenda, ningeweza kujaribu kufanya hivyo hapa. Lakini nafahamu kuna mjadala utafanyika kuhusu suala hilo. Ni vyema ukafika mwisho na ndipo hatua stahiki kama zipo zichukuliwe.”
Jibu hilo lilimfanya Mbowe aulize swali jingine huku akimshinikiza Waziri Mkuu ajiuzulu, lakini mbunge huyo wa Mlele mkoani Katavi, aliongeza: “Nirudie nilichosema. Suala la kujiuzulu kwangu si jipya. Bado nasisitiza tungoje tujadili hapa, tufike mwisho. Pengine huko nasi tutapata nafasi ya kuzungumza kidogo.”
Akisoma maoni na mapendekezo ya Kamati baada ya Mwenyekiti wake, Zitto kusoma sehemu ya uchambuzi wa sakata hilo juzi, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe alisema kwa uzito na unyeti wa suala hilo, Waziri Mkuu Pinda anapaswa kuwajibika kwa kauli zake na kwa kutotekeleza wajibu wake wa kikatiba ipasavyo, ilikurejesha imani ya wananchi kwa Serikali yao na viongozi wao wa kisiasa.
Kwa mujibu wa Filikunjombe, baada ya kupitia vielelezo vilivyomo katika ripoti ya CAG, “Kamati imejiridhisha pasipo mashaka kuwa, Waziri Mkuu, alikuwa na taarifa zote kuhusiana na mchakato mzima wa kuchotwa fedha kutoka katika akaunti ya Escrow.
Mbali ya Pinda, PAC pia imetaka kuwajibika kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Naibu wake, Stephen Maselle, Katibu Mkuu wao, Eliachim Maswi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kwa madai ya kuzembea katika majukumu yao ya kushindwa kuzuia uchotaji huo wa fedha hizo ambazo Serikali imesema si za umma.
Hata hivyo, kwa mujibu wa wabunge mbalimbali waliozungumza na gazeti hili pamoja na mijadala inayoendelea hapa, wanaona hoja ya Pinda aliyeingia madarakani Aprili 2008 baada ya kujiuzulu kwa Edward Lowassa kutokana na sakata la Richmond, inasukumwa zaidi na mapambano ya wanasiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwakani.
Pinda ni mmoja wa watu waliojipambanua kuwa anataka kumrithi Rais Jakaya Kikwete wakati muda wake wa kikatiba utakapomalizika mwakani, na nguvu inayotumika sasa, inaelezwa kuwa imelenga kumzima katika ndoto zake za kuwa Waziri Mkuu wa kwanza kushika wadhifa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pengine kwa kugundua au kuhisi hilo, Spika wa Bunge, Anne Makinda aliwaonya wabunge juzi kabla ya kuwasilishwa kwa taarifa ya PAC kuwa wajadili taarifa hiyo bila ya kuingiza hisia za Uchaguzi Mkuu ujao na ushabiki wa wagombea kwa kuwa rais ajaye Mungu pekee ndiye anayemjua.
Makinda alisema: “Tatizo lenu ninyi ndiyo mnaovunja kanuni maana mnaacha facts (hoja) na kuanza kujadili masuala yasiyohusiana. Hapa naomba mzingatie kuwa TBC inaonekana dunia nzima, hivyo watu wanawaangalia. “Niwaambie kuwa rais ajaye Mungu ndiye anayemjua na tayari ameshaandaliwa, sasa hakuna haja ya kuchafuana, kulipiza kisasi, kufiringana. Rais wa nchi hii Mungu anamjua ni nani, mnavyofanya ni kazi bure. Pia nawaomba muoneshe heshima kwa Mahakama kwa kadri inavyowezekana.”
Via habariLeo