Tuesday, 24 June 2014

Zungu: Mkuu wa Mkoa Dar hafai

Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu (CCM), amewashutumu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik na Mkurugenzi wa Jiji, Willison Kabwe, kulivuruga jiji hilo kwa kuwakamata wafanyabiashara ndogo ndogo (Wamachinga).

Shutuma hizo alizitoa jana bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa bajeti ya serikali ya mwaka 2014/2015 ambapo alisema viongozi hao wawili wametangaza vita dhidi ya wamachinga, mama na baba lishe kwa kupora bidhaa zao na kuwavunjia maeneo wanayofanyia shughuli zao za kujipatia kipato.

Zungu alisema viongozi hao wanafanya dhambi kubwa ya kuwaondoa mijini wafanyabiashara hao kwa njia zisizo halali ikiwemo kuwavunjia, kuwapora mali zao na kuwakamata hali inayosababisha umasikini kwa wahusika.

“Sadiq na Kabwe hawafai hata kidogo, wanachokifanya pale Dar es Salaam ni hatari kwetu maana wanaowaondoa wapiga kura wa katiba mpya na wa uchaguzi mkuu, wakiachwa waendelee na utaratibu wao tusidhani tutapata kura,” alisema.

Aliongeza kuwa uchafu wa Jiji la Dar es Salaam hautokani na wamachinga kwakuwa walikuwepo siku zote na jiji halikuwa safi, sasa wanashangazwa sababu zinazotolewa na Sadik na Kabwe kuwa kuwaondoa wafanyabiashara hao kutalifanya liwe safi.

Jiji halina mamlaka ya kutoa maagizo kwa halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam kama wanavyofanya, lakini wamekuwa wakikiuka utendaji wao kwa kuingilia kazi za manispaa husika.

Wiki iliyopita, Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu, naye alimshambulia Kabwe, kwa kudai alilivuruga Jiji la Mwanza, lakini ameshindwa kuwajibishwa na badala yake wamemuhamishia Dar es Salaam ili alivuruge zaidi.

“Mimi nilisema tangu mwanzo Kabwe ni janga, hamkunisikia, lakini sasa mmeanza kuona anavyotuvuruga kwa kuwaumiza wamachinga wetu na mambo mbalimbali yasiyo ya kiuungwana hata kidogo,” alisema.

Mbunge wa Mbarali, Modestus Kilifu (CCM), aliwatuhumu watendaji wa Wilaya ya Mbarali kuwatoza ushuru wakulima  wa mpunga kinyume na taratibu zilizopo na hivyo akatishia kuwa hawatakubali jambo hilo liendelee.

Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Lyimo (CHADEMA), alisema Rais Jakaya Kikwete hivi sasa amekuwa akiitwa Vasco Dagama kutokana na kusafiri mara kwa mara nje ya nchi.

“Hatukatai rais wetu asisafiri, lakini amezidisha, tena ana safari na idadi kubwa ya watu, apunguze ili fedha zitakazobaki zitumike kwenye shughuli za maendeleo kwa wananchi,” alisema