Tuesday, 13 May 2014

Tahadhali aliyoitoa JK juu ya ugonjwa wa dengue kwa watanzania

Wakati watu 400 wakithibitika kuwa na ugonjwa wa homa ya dengue, huku wengine watatu wakifariki dunia, Serikali imetoa taarifa kuhusu dalili za ugonjwa huo na namna inavyokabiliana nao. Mbali na kutoa taarifa hizo, Rais Jakaya Kikwete amewataka Watanzania popote walipo, wakipata dalili hizo, wasinywe dawa hovyo, badala yake waende kupima hospitali na kufuata ushauri wa kitaalamu.

“Naomba watu wakiona dalili za homa waende hospitali kupima maana hivi sasa kuna ugonjwa huu wa dengu…msinywe dawa tu bila kupima maana sasa unasambaa hivyo muende hospitali,” alisema Rais Kikwete.

Pia Rais Kikwete aliagiza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na Wizara ya Fedha, kuhakikisha kunakuwa na dawa pamoja na vifaa tiba vya kutosha kudhibiti ugonjwa huo, kwa kuwa ni wa dharura.

Dalili, aina Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo, alisema dalili za ugonjwa huo ni kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu na dalii hizo huanza kujitokeza kuanzia siku 3 hadi 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya dengue.

“Kwa wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana na dalili za malaria, hivyo basi tunawaomba wananchi wakipata homa kuhakikisha wanapima kama wana malaria au la, ili hatua stahiki zichukuliwe,” alisema Pallangyo.

Aliongeza kuwa kuna aina tatu tofauti za ugonjwa huo katika namna unavyojitokeza, iwapo mtu aking’atwa na mbu mwenye virusi hivu.

Aina ya kwanza ndio homa ya dengue yenyewe, ambayo huambatana na dalili kuu tatu za homa kali ya ghafla, kuumwa kichwa na maumivu ya viungo au uchovu.

Kwa Tanzania mpaka sasa zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa wamejitokeza wakiwa na dalili hizo. Aina ya pili ni dengue ya damu, ambayo huambatana na dalili za magonjwa kutokwa na damu kwenye fizi au puani na kutokwa na damu chini ya ngozi. Iwapo mgonjwa huyo ataumia sehemu yoyote, ni rahisi kupoteza damu nyingi kupitia kwenye michubuko.

Aina ya tatu ni dengue ya kupoteza fahamu, ambayo huambatana na mgonjwa kupoteza damu nyingi ambayo husababisha mgonjwa kupoteza fahamu. Mpaka sasa dalili hizo zimeonekana kwa mgonjwa mmoja kati ya wagonjwa 400 waliokwishwa thibitika kuwa na ugonjwa hapa nchini.

Via HabariLeo. Picha na Daily news