Polisi mjini Nairobi wanachunguza kisa cha mwanafunzi mmoja wa kidato cha tatu anayedaiwa kumuua mwenzake kwa kumchoma kisu.
Tukio hilo lilifanyika siku ya Jumatano mtaa wa Komarock viungani mwa mji wa Nairobi ambapo wawili hao inaelezwa kuwa walikuwa wanazozana juu ya msichana mmoja mpenzi wa mmoja wa vijana hao.
Maafisa hao wanamtafuta mtuhumiwa ambaye anadaiwa kumchoma Geoffery Onyango mwenye umri wa miaka 16 kisu kifuani alipokuwa akirudi nyumbani kutoka shuleni.
Wenzake wanasema kuwa wawili hao walikuwa na ugomvi kabla Onyango kuchomwa kisu.
Hatimaye alikimbizwa hospitalini lakini alifariki akipokea matibabu.
Mkuu wa Polisi mjini Nairobi alisema kuwa bado wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa huyo.