Baada ya waandaaji wa Tuzo za
Kilimanjaro Music (KTMA), kumuengua msanii, Ahmad Ally ‘Madee’ kutokana na wimbo wake wa ‘Tema Mate Tuwachape’
kukosa maadili, msanii huyo ameibuka na kusema hana tatizo na uamuzi huo, kwani maisha yake yataendelea kama kawaida.
Akizingumza jana, Madee alisema, kwa kawaida lazima utashtuka, lakini ndiyo tayari maamuzi yameshafanyika na hao walioamua wameshaamua, kwa hiyo hakuna tatizo.
Alisema maisha yanaendelea licha ya kwamba alipata taarifa kupitia vyombo vya habari kwamba, video ya wimbo huo ina matatizo na imefungiwa bila kupewa taarifa rasmi.
“Nilitarajia kuletewa barua rasmi kuwa video yako imefungiwa, mwisho wa siku leo napata taarifa kuwa wimbo wako umetolewa kwa sababu hauna maadili,” alisema Madee na kuongeza:
“Siwezi kuvunjika moyo, kwani kila siku nafanya kazi si kwa sababu ya tuzo hizo, hii si mara ya kwanza kushiriki kisha kutoka bila kupata kitu chochote, sijawahi kuvunjika moyo hata siku moja.”
Alisema, umewaambia wananchi
wachague nyimbo zilizofanya vizuri na wakachagua wimbo wao, halafu
unatolewa kwa madai hauna maadili, kulikuwa na haja gani ya kupigiwa kura.
Aliongeza kuwa lingekuwa jambo la
busara kwanza kuzitoa zile nyimbo
zinazoonekana kuwa na matatizo
mapema, kabla ya wananchi hawajatumia fedha zao kupiga kura.