Sunday, 12 June 2016

Wanafunzi wahaha Mbeya baada ya chuo kufungwa, baadhi yao wazimia

Takribani wanafunzi 2,000 wako njiapanda baada ya Chuo cha Mbeya Polytechnic kufungwa kwa madai ya kukiuka taratibu za uendeshaji.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amechukua hatua ya kukifunga chuo hicho jana kwa madai kuwa kinatoa mafunzo ya kilimo, huku kikiwa hakijapewa kibali na baadhi ya wanafunzi kudaiwa kusoma kozi kadhaa bila kuwa na sifa stahiki.

Makalla ameitaka menejimenti kuwarudishia wanafunzi fedha walizolipa kama ada. Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa chuo hicho aliwekwa chini ya ulinzi na hatimaye kuchukuliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi.

Wanafunzi walipatwa taharuki huku baadhi yao wakizimia baada ya agizo la Makallla la kukifunga chuo hicho ambacho awali kilikuwa kikijulikana kama Ihemi Polytechnic College.

Pamoja na gharama walizoingia, wanafunzi wanalalamikia muda waliopoteza kusoma masomo ambayo hayatambuliki na kuitaka Serikali walau kukubali vyeti ambavyo wamevitapa chuoni hapo.