Serikali imesema itaajiri jumla ya walimu 35,411 nchini katika shule za msingi na sekondari katika mwaka wa fedha 2016/2017 na kuonya kuwa watakaokaidi kwenda vijijini hawataajiriwa na serikali.
Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jaffo amesema hayo Bungeni alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF) aliyetaka kufahamu serikali inafanya nini kwawalimu waliopangiwa kwenda mikoa ya pembezoni, ikiwemo Lindi na kwingineko, lakini hawakuripoti.
Amesema uamuzi huo umetokana na serikali kupokea maombi mengi ya kazi kwa walimu, ambao mwaka jana hawakuripoti katika vituo walivyopangiwa pembezoni mwa miji kwa kutegemea kuajiriwa na shule binafsi, lakini hawakufanikiwa.
“Ni kweli kuna walimu wengi ambaohawakuripoti katika mikoa ya pembezoni na si Lindi peke yake, bali na mikoa mingine, ikiwemo Katavi na Kigoma,” ameongeza.
Ameongeza kuwa kwa mwaka huu, wataajiri walimu 35,411, lakini ambaye hataripoti katika mikoa hiyo na kuishia mjini tu, hataajiriwa tena serikalini, kama wanavyoombatena baada ya kukosa katika shule binafsi.