Tuesday, 25 November 2014

Vurugu la Escrow lazuia Kafulila kwenda fungate

Sakata la wizi wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, limesababisha Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila kutokwenda fungate baada ya kufunga ndoa mwishoni mwa wiki.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto alimpongeza kwa kufunga ndoa. Lakini, alimwomba mkewe Kafulila, Jessica Kishoa, kuwa mvumilivu kwa kuwa hawatakwenda fungate na mumewe hadi watakapomaliza kushughulikia suala la Escrow lililoko mbele yao.

Katika ibada hiyo ya ndoa iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Uvinza, Zitto alisema sakata la wizi wa fedha katika akaunti ya Escrow, ndicho kipaumbele chake sasa na atahakikisha suala hilo linafika mwisho.

Alisema kwa sasa amesimamisha mambo yake mengi, kuhakikisha anashughulikia suala hilo na kwamba amefanya hivyo kwa ajili ya maslahi ya Watanzania. Aliahidi kwamba lazima lifike mwisho.

Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe aliyekuwa mpambe wa Kafulila, alimpongeza kwa kukamilisha mchakato wa ndoa yake, licha ya kuwa katika kipindi kigumu cha kupigania maslahi ya Watanzania.

Filikunjombe alisema dhamira yao ni moja katika kutumikia Watanzania. Aidha, mbunge huyo alisema amemlea kiroho Kafulila na kuwataka wananchi wa jimbo la Kigoma Kusini, kumlea kisiasa awatumikie.

Kafulila alisema analo jukumu kubwa kuhakikisha suala la tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma kupitia akaunti ya Escrow, linafikia mwisho na kila mmoja anavuna alichopanda.

Wakati huo huo, jana Kafulila alihudhuria mkutano wa Bunge mjini Dodoma, ambako baada ya kuingia ukumbini, alikaribishwa kwa kushangiliwa na baadhi ya wabunge.