Friday, 14 November 2014

‘Kampuni za simu nchini zinawaibia wateja wao’

Naibu Waziri wa Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia, January Makamba amekiri kwamba kuna tatizo katika kampuni za simu nchini la kuwaibia wateja wao.

Makamba alikiri hilo jana wakati akijibu swali la nyongeza la  Mbunge wa Konde (CUF), Khatibu Said Haji.

Haji alisema wizi huo si mkubwa kama uliofanyika kwenye Escrow, bali ni wizi mdogo ambao wateja
wanaibiwa Sh2,000 au 3,000
katika simu zao.

“Mpemba wa Konde akiibiwa
Sh3,000, Mnyamwezi aliopo Tabora akiibiwa 2,000 ukizijumlisha ni mamilioni wanaibiwa Watanzania,”
alisema.

Alihoji Serikali inafikiriaje kuhusu gharama za kwenda kutoa malalamiko yao katika Mamalaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA).

Pia alitaka kufahamu ni nani aliopo nyuma ya pazia hilo au CCM ina fungu katika wizi huo? Akijibu, Makamba alisema CCM haihusiki na wizi huo unaotokana na kampuni za simu na kwamba chama hicho ni kizuri, makini na kimekuwa kikiaminiwa na wananchi.

“Napenda nikiri dhahiri tatizo la wizi na dhuluma lipo na ni kubwa na ndio zilisababisha tukaweka kanuni na hatua za kuchukua katika kudhibiti wizi huo,” alisema.

Pia alisema wateja wa vijijini
hawawezi kufuatilia madai yao
hadi Dar es Salaam, hali ambayo imeifanya Serikali kuanzisha kituo cha kushughulikia malalamiko
hayo.

“Sheria inazitaka kampuni kuweka huduma kwa wateja, lakini wakati mwingine utaratibu huo una matatizo, unaweza kupiga simu
hazipokewi, unaweza ukaambiwa usubiri lakini wakati ukisubiri unakatwa,” alisema.

Alisema katika kituo walichokianzisha, kutakuwa na
namba ya bure ya kupiga simu,
hali itakayomrahisishia mteja
kusafiri hadi Dar es Salaam kwa
ajili ya kulalamika.

Alisema kituo hicho kitakuwa
wazi saa 24, mteja atapewa namba atakapotoa lalamiko lake ili lishughulikiwe