Monday, 7 July 2014

Messi kama mchawi

Nasimuliwa na mashabiki wa Argentina kisa cha Lionel Messi kupewa unahodha wa timu ya taifa ya Argentina na kocha wao Alejandro Sabella. Ni kisa cha kumpatia mchawi mtoto wako ili akulelee.

Jumanne mashabiki wa Argentina walikuwa wamejaa katika mitaa ya Sao Paulo kwa ajili ya pambano lao dhidi ya Uswisi.

Katika treni wakati naelekea uwanjani nilikumbana nao na maswali yangu kwao yalihusu unahodha wa Lionel Messi katika timu yao.

Messi ni mpole. Sawa, anajituma uwanjani, lakini hana sifa kubwa za unahodha kushinda wachezaji wengine katika kikosi cha Argentina.

Amepewa unahodha kwa sababu ya ustaa wake. Achilia mbali sifa hizo, Messi anaonekana kuwa adui wa Waargentina wengi kwa sababu wanamwona kuwa ni Mhispania zaidi.

Kwa bahati ya mtende, nampata shabiki wa Argentina, Sergio Cuppitala ambaye anaongea lugha ya Kiingereza kwa ufasaha na anaonekana kuwa na upeo na masuala ya soka.

“Ilibidi unahodha apewe Messi. Ndiye staa zaidi katika timu, lakini kwa kumpatia unahodha Messi ilikuwa inamaanisha kwamba angebeba majukumu mengi katika timu ya taifa na hivyo kucheza kwa nguvu kama anavyocheza Barcelona,” anasema Cuppitala ambaye ni shabiki wa Boca Junior aliyewahi pia kuishi nchini Uholanzi.

“Messi hajulikani sana Argentina. Hata watu wa kwao Rosario hawakumfahamu kabla hajaanza kuwa staa Barcelona. Lakini unafanyaje wakati yeye ndiye mchezaji bora wa dunia mara nne mfululizo?” anasema Cuppitala.

“Wachezaji maarufu ndani ya Argentina ni Carlos Tevez, Martin Palermo, Rodrigo Palacios na wengineo.

Nakwambia Messi si maarufu sana. Wamemjua kupitia soka la Ulaya, lakini niamini mimi watu wa Argentina wanawaheshimu sana wachezaji waliopitia Boca Junior na River Plates, Messi hakupitia hizo timu,” anasema Cuppitala.

“Messi na Aguero ni marafiki sana. Kocha alikuwa anataka kuutumia urafiki wao kwa kupata Kombe la Dunia. Aliona Tevez angeharibu kwa sababu Tevez siyo rafiki wa karibu wa Messi wala Aguero. Hakutaka kuharibu kambi. Hakuna sababu nyingine zaidi ya hiyo,” alisema Cuppitala.

Via Mwananchi